*****
“Hakuna nchi iliyowahi kuendelea kwa kutegemea bajeti ya Serikali pekee”
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu, Ludovick Utouh, amesema mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) umekuwa ukipingwa kimyakimya na baadhi ya watendaji wa Serikali na mamlaka za mitaa kutokana na kuziba mianya ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.
CPA Utouh alitoa kauli hiyo Mei 9, 2026 alipokuwa akitoa mada kuhusu usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji katika Kongamano la Kitaifa la PPP kwenye Sekta ya Maji lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa msisitizo, Utouh alisema hakuna taifa lililowahi kufikia maendeleo ya kweli kwa kutegemea bajeti ya Serikali pekee bila kushirikisha nguvu ya uwekezaji kutoka sekta binafsi.
Alieleza kuwa mfumo wa PPP unaweka uwazi mkubwa katika utekelezaji wa miradi kwa sababu mwekezaji anayetoa fedha ndiye anayekuwa na usimamizi wa karibu wa matumizi na maendeleo ya mradi, hali inayopunguza mianya ya ubadhirifu iliyokuwa ikijitokeza katika baadhi ya miradi ya Serikali.
“PPP inapunguza kwa kiwango kikubwa mianya ya watu kufanya mambo yao kwenye miradi ya umma. Ndiyo maana unaona kuna maeneo mfumo huu haukubaliki kwa baadhi ya watu,” alisema Utouh.
Kwa mujibu wa CAG huyo mstaafu, changamoto nyingine inayokwamisha utekelezaji wa PPP nchini ni mtazamo hasi uliorithiwa kwa muda mrefu dhidi ya sekta binafsi, hali aliyosema imejengwa na historia ya siasa za ujamaa na kujitegemea zilizodumu kwa miaka mingi nchini.
“Bado kuna watu wanaamini sekta binafsi si sehemu sahihi ya maendeleo ya taifa. Lakini wakati huo huo tunasema sekta hiyo ichangie asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira yetu ya maendeleo. Hapo ndipo ninapoona kuna mgongano wa kimtazamo,” alisema.
Ili Tanzania ifikie malengo yake ya maendeleo, amesema ni lazima kuwe na mabadiliko ya fikra kuhusu nafasi ya sekta binafsi katika uchumi, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji, uwazi na uwajibikaji katika miradi ya PPP.
Mfumo wa ubia unaweza kuwa suluhisho muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, nishati, afya na miundombinu, hasa katika kipindi ambacho mahitaji ya uwekezaji yanaongezeka kuliko uwezo wa bajeti ya Serikali.



Post a Comment