Na Carlos Claudio, Dodoma.
Madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini yamehimizwa kuondoa tofauti zao na kushirikiana kwa pamoja katika kueneza neno la Mungu, ili watu wengi zaidi waweze kumjua Yesu Kristo na kupata neema ya wokovu.
Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Biblia Tanzania, Askofu Amos Muhagachi, wakati akiongoza tafakari ya neno la Mungu katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza kupitia Zaburi ya 133, Askofu Muhagachi alisema Chama cha Biblia Tanzania ni eneo muhimu linalowaunganisha Wakristo kutoka madhehebu mbalimbali, kwani kila dhehebu hukutana chini ya lengo moja la kueneza maandiko matakatifu.
“Mahali pekee ambapo kila mmoja anatakiwa kuungana ni katika Chama cha Biblia Tanzania, kwa sababu hapa hakuna tofauti za madhehebu bali kuna umoja wa kuhubiri neno la Mungu,” alisema Askofu Muhagachi.
Aidha, aliwahimiza Wakristo kujiunga na chama hicho na kuchangia huduma zake ili kusaidia kuendelea kusambaza Biblia kwa watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Biblia Tanzania, Askofu Dkt. Mark Malekana, akiwasilisha tathmini ya utendaji wa mwaka 2025, alisema chama hicho kimeendelea kupata mafanikio makubwa katika huduma zake za kueneza maandiko matakatifu.
Alisema kuwa kwa mwaka 2025, chama hicho kimefanikiwa kusambaza maandiko matakatifu 538,544, ikilinganishwa na maandiko 512,650 yaliyosambazwa mwaka 2024. Pia alisema idadi ya wanachama imeongezeka kwa wanachama 627, jambo linaloonesha kuimarika kwa mwitikio wa Wakristo katika kuunga mkono huduma hiyo.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Biblia Korea, aliyetoa salamu katika mkutano mkuu wa 40 wa chama hicho, alisema ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Korea umeendelea kuleta mafanikio makubwa katika kutimiza dhamira ya kueneza neno la Mungu kwa mataifa mbalimbali.
Alisema ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha maandiko matakatifu yanawafikia watu wengi zaidi nchini Tanzania na Korea.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki mkutano huo pia walitoa maoni yao, wakisema mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa katika kujenga umoja wa Kikristo pamoja na kuhamasisha ushiriki wa waumini katika kazi ya kueneza Injili.





Post a Comment