.........
Biharamulo.
BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, limewaagiza watendaji wa vijiji na kata kukaa kwenye vituo vyao vya kazi ili kusaidia usimamizi mzuri wa miradi ya umma.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha miundombinu iliyotengewa fedha na serikali kwa mwaka 2025/26 ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara, nyumba za watumishi pamoja na Zahanati.
Agizo hilo ni mkakati muhimu wa kuhakikisha thamani ya fedha (Value for Money) inaonekana katika miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Apolinary Mugarula, amesema watendaji wa kata na vijiji kuishi kwenye vituo vyao vya kazi kunalenga kuondoa mianya ya ubadhirifu na kuchelewa kwa miradi kutokana na usimamizi wa mbali.
Walikuwa kwenye kikao cha robo ya tatu cha kuwasilisha taarifa mbalimbali za kata, leo mei 6, 2026 kwa lengo la kupoke, kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo kwenye maeneo yao.
Ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara, na nyumba za walimu utasaidia kupunguza uhaba uliopo katika shule za msingi na sekondari.
Aidha ukamilishaji na ujenzi wa Zahanati na vituo vya afya unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi.
Vile vile wilaya ya Biharamulo inatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 143 (euro milioni 51) kwa ufadhili wa Serikali ya Hungary, utakaohitaji usimamizi wa karibu katika ngazi za vijiji.
Uamuzi wa Baraza hilo ambao umeungwa mkono na Madiwani wote akiwemo aliyeibua hoja hiyo kutoka Kata ya Nyamigogo, Elizeus Joseph, umesisitiza kuwa watendaji ambao watathibitika kutokuwepo kwenye vituo vyao vya kazi wahesabika kama wazembe kazini, kwani Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo wilayani humo.



Post a Comment