MAFANIKIO MAKUBWA ELIMU DODOMA YAVUTA HISIA KITAIFA

...........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa taaluma na maendeleo ya shule ili kuongeza ubora wa elimu nchini.

Akizungumza leo Mei 6, 2026 jijini Dodoma katika Mkutano wa Wadau wa Elimu Mkoa wa Dodoma, Prof. Shemdoe aliwataka viongozi katika ngazi zote kuhakikisha wanaweka malengo ya utekelezaji pamoja na mikakati madhubuti ya kuendeleza elimu, akitolea mfano mkakati uliowekwa na Mkoa wa Dodoma.

Amesema ni muhimu kudhibiti utoro wa walimu na wanafunzi, kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo ya shule pamoja na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuongeza tija katika sekta ya elimu.

“Napongeza jitihada zinazofanywa na walimu katika shule za serikali na zisizo za serikali katika kuhakikisha ufaulu unaendelea kuimarika katika mitihani ya kitaifa kuanzia darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili, cha nne na cha sita,” amesema Prof. Shemdoe.

Akiwasilisha takwimu za ufaulu, Waziri huyo amesema Mkoa wa Dodoma umeonyesha ongezeko kubwa la matokeo katika ngazi mbalimbali. 

Ufaulu wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 87.89 mwaka 2024 hadi asilimia 93.23 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 5.34.

Kwa upande wa darasa la nne, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 94.64 mwaka 2024 hadi asilimia 95.99 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.35. 

Aidha, matokeo ya kidato cha pili yamepanda kutoka asilimia 86.12 hadi asilimia 98.05, huku kidato cha nne kikiongezeka kutoka asilimia 92.81 hadi asilimia 94.49.

Katika kidato cha sita, ufaulu umeendelea kuwa wa juu zaidi kwa kuongezeka kidogo kutoka asilimia 99.86 mwaka 2024 hadi asilimia 99.87 mwaka 2025.

“Wanadodoma mmefanya kazi nzuri sana. Ushirikiano wenu umechangia mafanikio haya makubwa. Nawapongeza walimu wote pamoja na viongozi wa mkoa kwa juhudi zenu katika kuinua elimu,” ameongeza.

Prof. Shemdoe amesema walimu bora wataendelea kutambuliwa na kupewa zawadi ili kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mkoa huo umeandika historia mpya kwa kushika nafasi ya pili kitaifa mwaka 2025 katika matokeo ya elimu.


Amesema kabla ya miaka minne iliyopita, Dodoma haikuwahi kuingia hata katika kumi bora kwa zaidi ya miaka 12 hadi 20, lakini kwa sasa imepiga hatua kubwa kutokana na mikakati madhubuti na ushirikiano wa wadau wa elimu.

“Mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa mikakati tuliyojiwekea pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wadau wa elimu,” amesema Senyamule.

Ameongeza kuwa wadau wa elimu mkoani humo wameazimia kuhakikisha mipango na mikakati yote inayopangwa inatekelezwa kwa vitendo badala ya kubaki kwenye makabrasha.

Mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali wa elimu umeweka msisitizo katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana huku ukilenga kuongeza ubora wa elimu katika ngazi zote.





 

0/Post a Comment/Comments