MAGEREZA YAONYA UCHOMAJI MOTO MISITUNI, YAENDELEZA UZALISHAJI NA MAFUNZO KWA WAFUNGWA

.........

Na Carlos Claudio, Mbeya.

Jeshi la Magereza Tanzania limetoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na uchomaji moto wa misitu na mashamba ya miti katika maeneo yake, likieleza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha mazingira pamoja na uwekezaji mkubwa wa serikali uliowekwa katika sekta hiyo.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Kaimu Mkuu wa Gereza la Isupilo, ASP Anyosisye Mwashitete, amesema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni baadhi ya wananchi wanaoingia katika maeneo hayo kwa ajili ya kuwinda wanyama na kisha kusababisha moto unaoteketeza miti na mazao yaliyopandwa kwa juhudi kubwa.

Amesema licha ya changamoto hiyo, jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya magereza ili kuwajengea uelewa kuhusu athari za uchomaji moto. 

Amebainisha kuwa juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya wananchi wameanza kubadilika na kushirikiana kulinda rasilimali hizo.

Kwa upande wa uzalishaji, ASP Mwashitete amesema gereza la Isupilo linaendesha shughuli za kilimo cha miti ambazo hutumika kuzalisha mbao na nguzo, bidhaa muhimu katika maendeleo ya kiuchumi. 

Ameongeza kuwa miti hiyo huandaliwa kuanzia katika vitalu maalum kwa ushirikiano mkubwa na wafungwa, ambao hupata ujuzi wa namna bora ya kuitunza hadi inapokomaa.

“Wafungwa wanashiriki kikamilifu katika hatua zote za uzalishaji wa miti, kuanzia vitaluni hadi upandaji na utunzaji wake. Ujuzi huu unawasaidia wanapomaliza vifungo vyao ili waweze kujiajiri au kuajiriwa katika shughuli za kilimo na mazingira,” amesema.

Mbali na kilimo cha miti, pia gereza hilo linajihusisha na shughuli za ufugaji wa mifugo. ASP Mwashitete ameeleza kuwa wanafuga ng’ombe wa kisasa wa maziwa aina ya Friesian, Ayrshire na Jersey, pamoja na ng’ombe wa kienyeji aina ya crossbreed.

Amesema lengo la ufugaji huo ni kuwapatia wafungwa lishe bora pamoja na kuwajengea ujuzi wa kisasa wa ufugaji. Wafungwa hushiriki moja kwa moja katika shughuli za kuchunga, kuhudumia na hata kutibu mifugo hiyo chini ya uangalizi wa wataalamu.

Aidha, wamekuwa wakifundishwa mbinu za kukamua maziwa kwa mikono ili kuwawezesha kuwa na ujuzi watakaoutumia wanaporejea katika jamii baada ya kumaliza vifungo vyao.

Kwa ujumla, Jeshi la Magereza linaendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana katika kulinda mazingira na miradi ya maendeleo, huku likiendeleza dhamira yake ya kuwajengea wafungwa ujuzi utakaowasaidia kujitegemea na kuwa raia wema pindi wanaporejea uraiani.





 

0/Post a Comment/Comments