📍Ni ule wa kuboresha kituo cha kufua umeme
📍Amuagiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mradi huo
Na Mwandishi Wetu, Korogwe, Tanga
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange ameeleza kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi anayetekeleza mradi wa maboresho ya Kituo cha Kufua Umeme cha Hale kutokana na kuchelewa kukamilika kwa Mradi huo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2022.
Bw. Twange ameyasema hayo leo Mei 22, 2026 wakati wa ziara yake ya ukaguzi katika mradi wa Hale pamoja na mradi wa usafishaji wa bwawa la Mto Pangani iliyopo katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo amemtaka mkandarasi wa Mradi wa Hale kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuongeza wafanyakazi pamoja na muda wa kufanya kazi ili ukamilike kwa wakati.
“Siridhishwi sana na mwenendo wake. Mkandarasi amewahi kuomba nyongeza ya muda mara mbili na nimepata taarifa kuwa yuko kwenye hatua za kuomba nyongeza nyingine ya tatu. Ndio maana nimekuja kuona kuna nini,” amesema Bw. Twange.
Amesema mradi huo una maeneo saba ya utekelezaji ambapo maeneo mawili tayari yamekamilika huku mengine yakiendelea na utekelezaji.
“Nimezungumza na msimamizi wa mradi, mhandisi mshauri pamoja na mkandarasi na nimewaelekeza wakae pamoja kuhakikisha ifikapo mwisho wa mwezi Julai mradi huu uwe umekamilika,” amesema Bw. Twange
Aidha, kuhusu mradi wa usafishaji wa bwawa la Pangani, Bw. Twange amesema matarajio ya TANESCO ni kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.
“Matarajio yetu ni kutoupitiliza mwaka mmoja ili tumalize kabla ya msimu unaokuja wa mvua,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Bw. Twange amesema TANESCO kwa sasa inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya umeme nchini yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 13.4.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Mradi wa Hale Mha. Kulwa Byemelo amesema maagizo yaliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji yatatekelezwa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
“Mradi huu utakapokamilika utaimarisha upatikanaji wa umeme katika wilaya mbalimbali zinazochukua umeme kutoka kituo cha Hale pamoja na wilaya za Handeni, Muheza na Korogwe,” amesema Byemelo.
Ziara hii ni moja ya mikakati ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kubaini changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha zinatatuliwa kwa wakati na miradi ina kamilika ili watanzania waweze kuendelea kufurahia upatikanaji wa umeme wa uhakika.
<







Post a Comment