MGOGORO WA SOKO LA REHEMA NCHIMBI WAPATA UFUMBUZI DODOMA

.............

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu sakata la wafanyabiashara wa lililokuwa soko la Rehema Nchimbi, ikieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuwapatia maeneo mbadala baada ya kufungwa kwa soko hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 4, 2026 jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Halmashauri hiyo, Denis Gondwe, alisema kuwa uamuzi wa kufungwa kwa soko hilo ulitokana na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara kukosa maeneo rasmi ya kufanyia biashara.

Gondwe alifafanua kuwa Halmashauri ilichukua hatua ya awali kwa kupendekeza masoko mbadala yakiwemo Job Ndugai, Tambukareli, Makole na Kikuyu Kusini, ambayo kwa pamoja yalikuwa na uwezo wa kuhudumia takribani wafanyabiashara 297. 

Hata hivyo, alisema wafanyabiashara wengi walikataa maeneo hayo wakidai hayakukidhi mahitaji ya biashara zao.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya aliunda kamati shirikishi iliyojumuisha wadau kutoka serikalini na wawakilishi wa wafanyabiashara, kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu kupitia majadiliano ya pamoja.

Kupitia kamati hiyo, ilipendekezwa wafanyabiashara kuhamia eneo la Umonga lililopo mtaa wa Kitenge, kata ya Majengo, likitajwa kuwa na nafasi ya kutosha na lenye fursa nzuri kibiashara. Eneo hilo lina ukubwa wa mita za mraba 8,621.

Kwa mujibu wa Gondwe, Halmashauri imeandaa mpango wa uendelezaji wa awamu mbili katika eneo hilo, ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa vibanda vya muda ili kuruhusu wafanyabiashara kuanza shughuli zao huku maandalizi ya miundombinu ya kisasa yakiendelea.

Alibainisha kuwa tayari huduma muhimu zimekamilika katika eneo hilo, ikiwemo ujenzi wa choo cha kisasa na usawazishaji wa ardhi, hatua itakayowezesha biashara kuanza bila kuchelewa.

Katika utaratibu wa ugawaji wa maeneo, kila mfanyabiashara atapatiwa kiwanja chenye ukubwa wa mita tatu kwa tatu kwa ajili ya kujenga kibanda cha muda, kulingana na orodha iliyohakikiwa na kamati husika.

Hata hivyo, Gondwe alisema kikao cha kupitia rasimu ya mikataba kilichofanyika Aprili 27, 2026 kilishindwa kufikia muafaka baada ya wafanyabiashara kukataa kujadili ajenda iliyopangwa na badala yake kuibua hoja mpya, ikiwemo madai ya fidia na ongezeko la idadi ya wafanyabiashara.

Aidha, alitoa tahadhari kwa umma akisema hakuna mfanyabiashara yeyote aliyepewa au kuuziwa eneo kihalali katika eneo la Umonga hadi sasa. Alisisitiza kuwa mtu yeyote anayefanya malipo kabla ya kukamilika kwa taratibu rasmi anakuwa kwenye hatari ya kutapeliwa.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeeleza itaendelea kusimamia mchakato huo kwa uwazi, ushirikishwaji wa wadau na kuhakikisha wafanyabiashara wote wanapata maeneo halali ya kuendesha shughuli zao.


 

0/Post a Comment/Comments