.........
Na Carlos Claudio, Dodoma.
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetangaza rasmi kuanza kwa udahili wa wanafunzi wa ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2026/2027, huku likitoa tahadhari kwa waombaji kujilinda dhidi ya utapeli na kuhakikisha wanatunza taarifa zao binafsi kwa usalama.
Akizungumza jijini Dodoma Mei 28, 2026 wakati akitoa taarifa kwa umma, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda amesema dirisha hilo la udahili limefunguliwa rasmi kuanzia leo Mei 28 na litafungwa Julai 10, 2026.
Amesema udahili huo unahusisha kozi zote zinazosimamiwa na baraza hilo, huku NACTVET ikiwa imejipanga kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa uwazi, haki na usawa kwa waombaji wote wenye sifa stahiki nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Lingwanda, mifumo miwili itatumika kurahisisha maombi hayo kulingana na aina ya kozi na maeneo husika.
“Waombaji wa kozi za Afya na Sayansi Shirikishi kwa upande wa Tanzania Bara watatuma maombi yao kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (CAS) unaopatikana katika tovuti rasmi ya NACTVET,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa waombaji wa kozi zisizo za afya nchini kote pamoja na waombaji wa kozi za Afya na Sayansi Shirikishi kwa vyuo vya Zanzibar wanapaswa kuwasilisha maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo husika ndani ya kipindi hicho cha udahili.
Katika hatua nyingine, Dkt. Lingwanda ametoa onyo kali dhidi ya vitendo vya utapeli vinavyoweza kujitokeza wakati wa mchakato huo, akiwataka waombaji kufanya maombi yao binafsi bila kuwapa watu wengine taarifa zao muhimu.
“Ni muhimu kila mwombaji akahusika mwenyewe katika hatua zote za maombi, aweke taarifa sahihi na atunze namba ya simu aliyojisajilia bila kumshirikisha mtu mwingine ili kuepuka usumbufu usio wa lazima,” amesisitiza.
Amefafanua kuwa wanafunzi watakaochaguliwa watatumikiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) kutoka NACTVET wenye msimbo maalum wa siri ambao utatumika wakati wa kuripoti chuoni.
Baada ya usajili chuoni, wanafunzi hao pia watapaswa kufanya uhakiki wa taarifa zao kupitia mfumo wa ‘Student’s Information Verification’ uliopo kwenye tovuti ya baraza hilo.
Sambamba na hilo, Katibu Mtendaji huyo amewashauri waombaji na jamii kwa ujumla kupakua Kitabu cha Mwongozo wa Udahili wa mwaka 2026/2027 ili kupata taarifa sahihi kuhusu vyuo vilivyosajiliwa pamoja na kozi zinazotolewa.
Wakati huo huo, NACTVET imevitaka vyuo vyote nchini kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na baraza hilo wakati wote wa zoezi la udahili ili kuendelea kulinda ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini.


Post a Comment