POLISI DAR: DJUMBE APATIKANA, UCHUNGUZI WAENDELEA KUWABAINI WALIOMKAMATA



 ****

Na Mwandishi Maalum,Dar

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio la kukamatwa kwa David Joseph Mghanja maarufu kama Djumbe, kufuatia taarifa zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zikidai alichukuliwa na watu wasiojulikana maeneo ya Bunju.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 21, 2026 na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Jeshi hilo lilianza kufuatilia tukio hilo tangu usiku wa Mei 20, 2026 baada ya taarifa mbalimbali kuanza kusambaa mtandaoni.

Katika ufuatiliaji huo, Polisi walifanikiwa kulipata gari lenye namba T 609 DTD aina ya Toyota Wish rangi nyeusi, linalomilikiwa na Allan Elisonguo Macha, ambalo inadaiwa Djumbe alikuwa akisafiria kama abiria wakati alipokamatwa na watu wanaodaiwa kutokujitambulisha.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa asubuhi ya leo Mei 21, 2026, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa zikidai kuwa Djumbe alikuwa katika Ofisi za Chadema zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Amesema Askari walifika katika eneo hilo lakini hawakumkuta, huku wakimkuta mtu anayedaiwa kuwa alikuwa pamoja naye wakati wa tukio la kukamatwa kwake.

Aidha, Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa Djumbe tayari amepatikana salama na kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini watu waliomkamata pamoja na sababu za kufanya tukio hilo.

Polisi wameeleza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mishoo

0/Post a Comment/Comments