...........
Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limeungana na wafanyakazi wengine nchini na duniani kote kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi kwa kutembelea na kutoa msaada wa kibinadamu katika shule ya watoto wenye mahitaji maalumu ya Mitindo, iliyopo wilayani Misungwi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mabatini, Wilaya ya Nyamagana mkoani humo, Mrakibu wa Polisi (SP) Daktari Steven Kisaka, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, amesema wao kama kikosi cha afya wametoka ofisini na kwenda kukutana na kundi lenye mahitaji maalumu na kutoa msaada ikiwa ni utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii.
"Leo, Siku ya Wafanyakazi, tumetoka maofisini kwa ajili ya kukutana na jamii. Tumezoea jamii inakuja kwetu kutibiwa, lakini leo tumetoka sisi kwenda kuifuata jamii," alisema Dkt. Kisaka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Elimu Maalumu ya Mitindo, Januari Gunze, amelishukuru Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali, zikiwemo za ulinzi pamoja na mahitaji muhimu ya makundi yaliyopo katika shule hiyo.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada walioutoa pamoja na kuendelea kuimarishiwa usalama wao.
"Sisi tukiwa tumekaa maeneo haya, kimsingi tupo mbali na wazazi wetu, lakini ninyi kuja kwenu kwenye kituo hiki mmeonyesha kuwa ni wazazi," alisema Hassan Suleiman.
"Tunalishukuru sana Jeshi la Polisi kwa kutuimarishia ulinzi," alisema Abigael Jeremia.
Post a Comment