PPP YALETA MAPINDUZI KATIKA HUDUMA ZA HIJJA MAKKA - KAFULILA


 ******

Mkurugenzi Mtendaji wa PPP-Centre, David Kafulila kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa X, amesema mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) umeleta mageuzi makubwa katika huduma za Hijja nchini Saudi Arabia kwa kuongeza ufanisi na kupunguza adha kwa mahujaji.

Akitoa salamu za Eid al-Adha kwa Waislamu duniani, Kafulila amesema moja ya mafanikio makubwa ya PPP ni maboresho yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Abdulaziz (KAIA) uliopo Jeddah, unaotumiwa na mamilioni ya mahujaji wanaoelekea Makka.

Amesema kabla ya maboresho hayo, mahujaji walikuwa wakitumia kati ya saa sita hadi 10 kukamilisha taratibu za uwanjani, lakini baada ya utekelezaji wa mradi wa PPP wenye thamani ya dola milioni 249, muda huo umepungua hadi dakika 45 na saa moja.

“PPP imeongeza ufanisi mkubwa sana. Kabla ya mradi huu, uwanja ulikuwa ukihudumia wastani wa mahujaji milioni moja kwa mwaka, lakini sasa unahudumia kati ya abiria milioni nane hadi tisa kwa mwaka,” amesema Kafulila.

Kafulila amefafanua kwamba, mradi huo ulitekelezwa kupitia mkataba wa miaka 20 kati ya Mamlaka ya Anga ya Saudi Arabia (GACA) na kampuni binafsi ya Hajj and Umrah Terminals Development Company, ukihusisha Saudi Binladin Group pamoja na Aéroports de Paris Management huku Shirika la IFC likiwa mshauri mwelekezi.

 Mafanikio hayo yanapaswa kuwa somo kwa Tanzania katika kuendeleza sekta ya usafiri wa anga na miundombinu mingine kupitia uwekezaji wa PPP.

“Tusiogope kuwakaribisha wawekezaji kupitia PPP kwenye viwanja vyetu vya ndege ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuchochea mageuzi ya kiuchumi,” amesema.

Aidha, amesema tathmini ya usafiri wa anga duniani ya mwaka 2023 inaonyesha kuwa licha ya viwanja vya ndege vinavyoendeshwa kwa PPP kuwa asilimia 14 pekee duniani, vinahudumia karibu asilimia 40 ya abiria wote duniani.

“PPP na ufanisi ni pacha,” amesema Kafulila huku akiwatakia Waislamu wote Eid Mubarak yenye amani na baraka.

0/Post a Comment/Comments