PUMA ENERGY KUZINDUA PROGRAMU YA PRIS KUWAZAWADIA WATEJA


Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah,akizungumza j jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari.
******

Kampuni ya Puma Energy Tanzania leo inatarajia kuzindua rasmi programu ya PRIS App, mfumo maalumu wa kidijitali unaolenga kuwazawadia wateja wanaofanya manunuzi ya mafuta, vilainishi pamoja na bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika maduka ya kampuni hiyo nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu matumizi ya programu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah alisema mpango huo ni sehemu ya kuimarisha huduma kwa wateja kupitia teknolojia ya kidijitali.

Alisema kampuni hiyo inaunga mkono Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha kidijitali kikanda kwa kuboresha miundombinu, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi.

“Programu hii inalenga kurudisha thamani kwa wateja wetu kwa kuwapatia zawadi wanapofanya manunuzi katika vituo vyetu,” alisema Abdallah.

Alisema Puma Energy inaendesha zaidi ya vituo 2,201 vya rejareja na kuhudumia viwanja vya ndege 107 duniani, huku ikiwa na mpango wa kuongeza idadi hiyo maradufu ifikapo mwaka 2030 ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Puma Energy Tanzania imechangia zaidi ya Sh trilioni 1.4 kwa Serikali kupitia kodi na ushuru mbalimbali.

Aliongeza kuwa mwaka 2025 kampuni hiyo ilitangaza gawio la Sh bilioni 21, hatua iliyoongeza mapato yatokanayo na umiliki wa asilimia 50 wa Serikali kupitia Msajili wa Hazina.

Kwa mujibu wa Abdallah, baada ya uzinduzi wa mafanikio wa PRIS App katika nchi za Zimbabwe, Malawi na Botswana, Tanzania sasa inakuwa soko la nne barani Afrika kuzindua mfumo huo.

Pia alisema kampuni hiyo kwa sasa inatoa huduma ya mafuta ya ndege katika viwanja nane vya ndege nchini, vikiwemo viwanja vitatu vya kimataifa, huku akisisitiza kuwa mafuta yanapatikana kwa kiwango cha kutosha kuhudumia mahitaji ya Watanzania.





Bi. Lilian Kanora, Meneja Masoko Puma Energy Tanzania.

Bw. Sulpis Mmasi, Meneja Mauzo ya Rejareja Puma Energy Tanzania.

0/Post a Comment/Comments