📌 Asisitiza ushirikiano wa kikanda kupitia miradi ya umeme na ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta
Rais wa Kenya,Mhe. William Ruto amesema kuwa miradi ya pamoja ya nishati kati ya Tanzania na Kenya inaendelea kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Akilihutubia Bunge la Tanzania kwa mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Mei 05,2026 Mhe. Ruto ametaja
mafanikio ya mradi wa umeme wa Kenya–Tanzania Power Interconnector wa msongo wa kilovolti 400 uliohusisha njia ya usafirishaji umeme ya zaidi ya kilomita 500.
Amesema mradi huo haujaishia tu kuunganisha gridi za umeme, bali pia umesawazisha mifumo ya umeme kati ya nchi hizo mbili, umewezesha biashara ya umeme, umeongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.
Rais Ruto ameongeza kuwa mipango ya mradi mpya wa kuunganisha umeme kupitia njia ya Shinyanga–Mabuki- Kilgoris- Rongai Kenya itaongeza zaidi uwezo wa usafirishaji wa umeme na kuimarisha soko la pamoja la nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.
‘Ushirikiano huu utasaidia kutumia vyema rasilimali mbalimbali za nishati zilizopo ukanda huu, ikiwemo gesi ya Tanzania, nishati ya jotoardhi pamoja na vyanzo vingine vya nishati jadidifu ili kujenga soko la nishati lenye ushindani na uhakika zaidi.
Katika hatua nyingine, Rais Ruto amepongeza uamuzi wa Uganda kuwekeza katika Kampuni ya ujenzi wa bomba la mafuta ya Kenya akisema hatua hiyo imeibadilisha nchi hiyo kutoka mtumiaji hadi mshirika na kufanya miundombinu hiyo kuwa mali ya pamoja ya kikanda.
Aidha ameeleza kuwa Kenya iko tayari kuwa mshirika wa kimkakati katika mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta (refinery) mkoani Tanga, akibainisha kuwa licha ya awali kutamani mradi huo ujengwe Mombasa, kijiografia Tanga iko karibu na nchi hiyo hivyo ni sehemu sahihi mradi kutekelezwa.




Post a Comment