Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema uzinduzi wa Mfumo wa Kidijitali wa Huduma za Mafuta wa PRIS ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia ndani ya sekta ya mafuta.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Puma Retail Information System katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Makamba amesema mfumo huo utasaidia kusimamia mauzo, malipo, stoki za mafuta pamoja na taarifa za biashara kwa wakati halisi.
Amesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya nishati yataongeza ufanisi, uwazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.
Aidha, ameipongeza Puma Energy Tanzania kwa kuendelea kuwekeza nchini kupitia mifumo ya kidijitali, upanuzi wa vituo vya mafuta pamoja na uwekezaji katika nishati safi ya CNG.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah alisema mpango huo ni sehemu ya kuimarisha huduma kwa wateja kupitia teknolojia ya kidijitali.
Alisema kampuni hiyo inaunga mkono Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Kidijitali Tanzania wa mwaka 2024 hadi 2034, unaolenga kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha kidijitali kikanda kwa kuboresha miundombinu, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi.







Post a Comment