RC MTWARA: CCM INA JUKUMU LA KUHAMASISHA WAKULIMA KUONGEZA TIJA KUPITIA MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA

 

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanal Donald Msengi, amewashauri Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwahimiza wakulima kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuleta mabadiliko chanya kiuchumi na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

Akizungumza  wakati wa Mafunzo ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa Viongozi wa Chama na Serikali kutoka mkoa wa Dodoma yaliyofanyika mkoani Mtwara, Kanal Msengi amesema mfumo huo umeleta mafanikio makubwa kwa vyama vya ushirika mkoani humo kwa kuviwezesha kuwa imara kiuchumi. Ameeleza kuwa kupitia mfumo huo, vyama vimefanikiwa kufanya uwekezaji mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maghala, ununuzi wa magari, uanzishaji wa viwanda pamoja na kuchangia huduma za kijamii kama elimu, afya na maji.

“Ni muhimu viongozi mkatumia nafasi zenu kuwahamasisha wakulima na wanaushirika kutumia mfumo huu, kwani umeleta manufaa makubwa na una uwezo wa kuleta mageuzi chanya kwa sekta ya kilimo,” amesema Kanal Msengi.

Naye Kaimu Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara, Robert Nzunza, amebainisha hatua muhimu za mchakato wa stakabadhi za ghala kuwa ni pamoja na maandalizi ya msimu wa mauzo, ukusanyaji wa mazao ghalani, usafirishaji wa mazao kwenda ghala kuu, mapokezi ya mazao, mauzo kupitia minada ya mtandao, malipo ya fedha kupitia vyama vikuu (Unions), malipo kwa wakulima na wadau, pamoja na utoaji wa mizigo ghalani.

Kwa upande wake Mkuu wa msafara huo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka mkoa wa Dodoma, Donald Mejetii, amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo viongozi hao ili waweze kuwahamasisha wakulima wa Dodoma kutumia mfumo huo kwa tija zaidi.

Viongozi wa Chama na Serikali kutoka mkoa wa Dodoma wapo mkoani Mtwara kwa ziara ya kujifunza Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika vyama vya ushirika na namna unavyoweza kuinua kipato cha mkulima. Katika ziara hiyo pia wametembelea Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU LTD pamoja na Chama cha Msingi Mayanga AMCOS.

0/Post a Comment/Comments