Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kamishna Mstaafu wa Uhifadhi, Mhe. William Mwakilema, amesema Serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya nishati ya umeme ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga katika hafla ya kukabidhi mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa katika Kata ya Mpale leo Mei 6, 2026, DC Mwakilema ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kufanikisha ujenzi wa mradi huo mkubwa kwa sasa ambao umekabidhiwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya usambazaji kwa wananchi.
Amesema kufikishwa kwa umeme wa huo katika vitongoji vya Ubiri, Kwemuhoyo, Milongwe, Kweulasi na Kwemhole ni hatua muhimu itakayosaidia kukuza shughuli za uzalishaji mali, biashara na huduma za kijamii, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia utekelezaji wa mradi huo ambao umeleta suluhisho la kudumu la umeme katika eneo hilo.
Halikadhalika Balozi Kingu amesisitiza umuhimu wa wananchi kuutumia umeme huo kuanzisha miradi ya maendeleo pamoja na kuchangamkia fursa za nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira.
Naye, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wa maeneo ya vijijini na sehemu za pembezoni mwa miji wanapata umeme wa uhakika.
Mha. Olotu ameongeza kuwa kabla ya kufikishwa kwa umeme wa gridi ya taifa, eneo hilo lilikuwa linatumia umeme wa jua kupitia kampuni ya Watu na Umeme tangu mwaka 2017 lakini Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 ilielekeza Serikali kubadilisha mfumo huo na kupeleka umeme wa gridi ya taifa ili kuwezesha matumizi makubwa zaidi ya umeme zitakazosaidia kuendesha mashine za viwandani na huduma nyingine muhimu.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Watu na Umeme Ltd, Dkt. Prosper Magali, amesema mradi wa awali wa umeme wa jua ulianza mwaka 2014 na uliweza kuhudumia kaya 254, lakini mahitaji ya sasa yameongezeka na hivyo kuhitaji umeme wa gridi.
Dkt. Magali ameishukuru REA kwa kushirikiana mkubwa hadi kufanikisha hatua ya sasa ya kukabidhi miundombinu hiyo TANESCO ambayo inakwenda kuboresha huduma kwa wananchi.
Mradi huo unatajwa kuwa ni hatua kubwa ya maendeleo kwa wakazi wa Vitongoji vya Mpale, ambapo sasa wanatarajia kunufaika na umeme wa uhakika utakaowezesha ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha yao.








Post a Comment