Serikali Yaanza Rasmi Upanuzi wa Barabara ya Dodoma–Chamwino kuwa Njia Sita

.........

Na Ester Maile Dodoma 

Waziri wa Ujenzi Abdallah Hamisi Ulega  ameongoza hafla ya utiaji saini wa mkataba wa upanuzi wa barabara ya Dodoma hadi Chamwino yenye urefu wa kilomita 32 kuwa njia sita, hatua inayotajwa kuwa mkombozi mkubwa wa usafiri na maendeleo ya kiuchumi katika makao makuu ya nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri amesema mradi huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha kisasa cha biashara, uwekezaji na huduma za kijamii huku ukiondoa changamoto ya msongamano wa magari unaoendelea kuongezeka kila siku.

“Barabara hii siyo tu njia ya kupita magari, bali ni daraja la maendeleo kwa wananchi wa Dodoma na Watanzania wote. Kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji, kuongeza usalama barabarani na kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema Waziri.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza kasi ya usafiri kati ya Dodoma na Chamwino, kuvutia wawekezaji zaidi pamoja na kuboresha mandhari ya mji mkuu unaokua kwa kasi.

Wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wameeleza matumaini yao kuwa mradi huo utafungua fursa mpya za ajira, biashara na huduma bora za usafiri katika ukanda huo muhimu wa kitaifa.








 

0/Post a Comment/Comments