Na Carlos Claudio , Dodoma
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na Tanzania Official Seed Certification Institute (TOSCI) katika kufanya ukaguzi na usimamizi madhubuti wa mbegu zinazoingizwa nchini, ili kudhibiti wimbi la mbegu feki zinazozalishwa mipakani na kuingizwa kinyemela nchini.
Silinde amesema uwepo wa mbegu zisizo na ubora unadhoofisha uzalishaji wa mazao, kuwarudisha nyuma wakulima na kuhatarisha juhudi za taifa za kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na maendeleo ya sekta ya kilimo.
Akizungumza katika Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu, Silinde amesema Serikali haitavumilia biashara ya mbegu feki kwa kuwa zimekuwa chanzo cha kupungua kwa uzalishaji wa chakula na hasara kwa wakulima wengi nchini.
Aidha, ameisisitiza TOSCI kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu zilizokaguliwa na zenye nembo rasmi ya taasisi hiyo, ili kuwasaidia wakulima kutambua mbegu halali na kuepuka bidhaa bandia zinazoharibu uzalishaji.
“Ni muhimu pia kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora ili kuhakikisha upatikanaji wa mbegu zenye ubora wa uhakika kwa wakulima,” amesema Silinde.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amezitaka taasisi za kifedha pamoja na mabenki kuweka mifumo rafiki ya mikopo yenye riba nafuu kwa wazalishaji wa mbegu na wakulima, ili waweze kumudu gharama za teknolojia mpya zinazosaidia kuongeza uzalishaji.
Amesema sekta ya mbegu inahitaji uwekezaji mkubwa wa mitaji, hasa katika miundombinu ya umwagiliaji na uchakataji wa mbegu, hivyo ushiriki wa taasisi za fedha ni muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya kilimo ya mwaka 2030 pamoja na Agriculture Master Plan 2050.
“Tunaamini taasisi zote za fedha hapa nchini lazima zilichukulie jambo hili kwa uzito ikiwa ni sehemu ya kutimiza malengo ya taifa katika maendeleo ya kilimo,” amesema.
Silinde pia amewataka wabia wa maendeleo wakiwemo Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA) kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kusaidia kujenga uwezo wa kitaasisi, tafiti pamoja na maboresho ya sera za sekta ya mbegu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Yustina Rahhi, ameishauri TOSCI kuongeza uzalishaji wa mbegu bora zinazoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbegu bora ili kuongeza tija mashambani.



Post a Comment