******
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa gawio la Sh bilioni 8.38 kwa Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 kutoka Sh bilioni 5.58 zilizotolewa mwaka 2024.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa jijini Dar es Salaam leo, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema mafanikio hayo yanaonyesha benki hiyo inaendelea kuimarika na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Mchechu amesema Serikali itaendelea kuiongezea mtaji TADB kutokana na umuhimu wake katika kukuza kilimo, mifugo na uvuvi, sekta ambazo zinaajiri idadi kubwa ya Watanzania na kuchangia uchumi wa taifa.
Alisema hadi sasa Serikali imewekeza mtaji wa Sh bilioni 452.37 katika benki hiyo, huku akibainisha kuwa faida kabla ya kodi imeongezeka kutoka Sh bilioni 24.68 mwaka 2024 hadi kufikia Sh bilioni 35.45 mwaka 2025.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TADB, Ishmael Kasekwa amesema bodi itaendelea kuisimamia benki hiyo kwa weledi ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanaendelea kutimia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TADB, Ishmael Kasekwa, Akizungumza na Waandishi wa Habari Mapema Leo jijini Dar es salaam.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema faida baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia 50 kutoka Sh bilioni 18.61 mwaka 2024 hadi Sh bilioni 27.94 mwaka 2025 kutokana na kuongezeka kwa utoaji wa mikopo.
Nyabundege amesema kitabu cha mikopo kimeongezeka kutoka Sh bilioni 534.16 hadi Sh bilioni 806.75, huku thamani ya mali za benki ikifikia Sh trilioni 1.3. Aliongeza kuwa TADB imefungua ofisi mpya za mikoa Kigoma, Kagera na Ruvuma ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege Akizungumza na Waandishi wa Habari Mapema Leo jijini Dar es salaam.
picha ya pamoja za pamoja baada ya kuzungumza na Waandishi wa Habari pamoja na m Mkuu wa Wanahisa jijini Dar es Salaam leo.











Post a Comment