TANESCO YAHARAKISHA MRADI WA UMEME WA BILIONI 514 DODOMA

...........

Na Carlos Claudio, Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania, TANESCO limesema ujenzi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma umefikia asilimia 82.5 huku serikali ikiagiza kazi hiyo ikamilike ifikapo Agosti 18 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo katika kituo cha kupooza umeme cha Zuzu.

Amesema mradi huo ni sehemu ya muendelezo wa usafirishaji wa umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere kwenda maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Twange amesema maboresho makubwa yanaendelea katika kituo cha Zuzu ili kuongeza uwezo wa kupokea umeme mkubwa utakaotoka Chalinze kuelekea Dodoma.

“Mahitaji ya umeme yanaongezeka kutokana na ongezeko la watu, uwekezaji mkubwa pamoja na mahitaji ya taasisi mbalimbali za serikali, shule, hospitali na sekta nyingine, hivyo tunapaswa kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa imara zaidi,” amesema.

Ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa mradi huo, serikali ilisaini mkataba wa nyongeza na mkandarasi ili kuhakikisha kazi zinakamilika mapema kabla ya muda uliokuwa umepangwa awali.

Kwa mujibu wa Twange, ukaguzi uliofanyika kuanzia Dumila hadi Dodoma umebaini kuwa vifaa vya kutosha vipo eneo la mradi na mkandarasi ameongeza wataalamu ili kuharakisha utekelezaji wa kazi.

“Tuna uhakika kwamba ifikapo Agosti 18 mwaka huu mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma pamoja na maboresho ya vituo vya kupooza umeme vya Chalinze na Dodoma utakuwa umekamilika,” amesema.

Amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya TBEA kutoka China na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 514 za Kitanzania.

Aidha amesema mradi huo wa kimkakati utaongeza uwezo wa usafirishaji wa umeme nchini na kuwanufaisha wakazi wa Dodoma pamoja na maeneo mengine ya Tanzania.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Newton Livingstone amesema mradi huo wenye urefu wa kilomita 345 unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema hadi sasa kazi zinaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na upanuzi wa vituo vya kupooza umeme vya Chalinze na Dodoma.

“Kazi ipo salama na matarajio yetu ni kuhakikisha mradi unakamilika mwezi wa nane kama ilivyopangwa,” amesema.









 

0/Post a Comment/Comments