TARURA YAPATA DOLA MILIONI 65 KUTEKELEZA MIRADI YA DHARURA

*******

Serikali imeiwezesha Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupata dola milioni 65 kwa ajili ya utekelezaji wa matengenezo ya miundombinu ya barabara kupitia mfuko wa dharura (CERC).

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala huo katika mradi wa ujenzi wa daraja lenye urefu wa Mita 22 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa Mita 290 kwenye  barabara ya Ndovelwa yenye urefu wa Km. 20.2 katika Manispaa ya Tabora.

Mhandisi Seff amesema fedha hizo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia uliotolewa kufuatia tathmini ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua za El-Nino za mwaka 2024.

Amesema  tathmini hiyo ilibaini maeneo mengi ya barabara yaliyoharibiwa na hivyo kuhitaji matengenezo ya haraka ili kurejesha mawasiliano na huduma kwa wananchi.

“Miradi hii inatekelezwa nchi nzima na kwa wastani utekelezaji wake umefikia asilimia 70. Kazi zote zinatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2026,” Alisema.

Aidha, amesema  miradi hiyo inatekelezwa na makandarasi wazawa huku akiwasisitiza Mameneja na wasimamizi wa TARURA nchini kuongeza usimamizi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.

Akizungumzia ujenzi wa daraja hilo, Mhandisi Seff amesema ameridhishwa na ubora wa kazi inayoendelea na kusisitiza kuwa miundombinu inayojengwa inapaswa kudumu na kupitika wakati wote ili kuwawezesha wananchi kufikia masoko, shule na kusafirisha pembejeo za kilimo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA Bi. Nunu Mangu amesema  ujenzi wa daraja na barabara hizo utasaidia kufungua mawasiliano kwa wananchi wa maeneo husika na kuhakikisha usafiri unakuwa wa uhakika katika misimu yote ya mwaka.

Pia aliwataka wananchi kuitunza miundombinu inayojengwa kwa kuwa Serikali kupitia TARURA inaendelea kuwekeza fedha nyingi kuboresha miundombinu nchini.



 

0/Post a Comment/Comments