BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam limeonya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maendeleo kuhakikisha wanamaliza kazi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, likisema halitakuwa tayari kuvumilia ucheleweshaji wa miradi muhimu kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha baraza hilo kilichopokea taarifa ya robo ya tatu ya mwaka 2025/26, Mstahiki Meya wa Temeke, Uzairu Athumani, alisema manispaa hiyo itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo.
Alisema madiwani wamejadili utekelezaji wa miradi katika sekta za elimu, afya, barabara, usafi wa mazingira pamoja na miundombinu, huku wataalamu wakitakiwa kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa yanatekelezwa haraka.
Uzairu alisema Temeke imeamua kuwapa nafasi kubwa wakandarasi wazalendo ili kusaidia kukuza uchumi wa ndani, huku akisisitiza kuwa wananchi wanaolipa kodi ndio msingi wa maendeleo ya halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine, Manispaa ya Temeke imetangaza kutumia zaidi ya Shilingi bilioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa hospitali na shule za ghorofa 10.
Aidha, halmashauri hiyo imesema imefikia hatua ya kuvunja mkataba wa mkandarasi wa mradi wa Shule ya Sekondari Chang’ombe baada ya kushindwa kuendeleza ujenzi wa jengo la ghorofa tano ambalo hadi sasa halijafikisha hata asilimia 50 ya utekelezaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomaary Satura, alisema manispaa hiyo inaendelea na utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 10 wenye lengo la kutatua changamoto za miundombinu na kuboresha huduma kwa wananchi.
Satura alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa tozo maalumu kwa malori kuanzia mwezi Julai ili kusaidia kupunguza msongamano pamoja na kuongeza mapato ya halmashauri, huku madiwani wakisisitiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya wakandarasi wazembe.



Post a Comment