Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa
kushirikiana na shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO)
imetangaza rasmi ushirikiano wa Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga
kuhamasisha kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii
kuhusu changamoto za matukio ya hali mbaya ya hewa, na utoaji wa tahadhari za
mapema, na usalama kwenye maji hapa Tanzania.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden, Jijini Dar -Es -Salaam, Bi. Mary
Francis Mahemba, Afisa Uchechemuzi (Advocacy Officer) kutoka Shirika la
Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo - EMEDO alisema kuwa vyombo vya habari vina
nafasi muhimu katika kuifikia jamii kwa taarifa sahihi zinazoweza kusaidia
kuokoa maisha, kupunguza athari za majanga yanayohusiana na hali ya hewa, pamoja
na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu usalama majini.
“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika
kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu tahadhari za
hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga. Kupitia
tuzo hizi tunatambua mchango wao katika kujenga jamii salama na inayotambua
hatari za kuzama maji,” alisema Bi. Mary Francis Mahemba.
Amesema kuwa Tuzo hizo zinalenga kuhamasisha
utayarishaji wa habari zenye ubora kuhusu Matukio ya hali mbaya ya hewa na
athari zake kwa jamii;Tahadhari za mapema za hali ya hewa;Usalama wa vyombo vya
usafiri na usafirishaji kwenye maji ,Uzuiaji wa ajali na vifo vitokanavyo na
kuzama maji,Ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya
hewa.
Kwa muktadha huu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
kwa kushirikiana na Shirika la EMEDO wameandaa Tuzo zitakazowahusisha waandishi
wa Habari. Tuzo hizo zitahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali
vya redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali
nchini Tanzania. Waandishi wanaalikwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au
kurushwa hewani ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe 1/08/2025 mpaka
tarehe 30/08/2026. Kazi zote zitumwe kwenye barua pepe hizi mbili media@meteo.go.tz
/ mediahaliyahewa@gmail.com
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania Bi. Monica Mutoni, Meneja Masoko na Uhusiano, alisisitiza
umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema
katika kuokoa maisha ya wananchi, hususan wale wanaotegemea shughuli za maji
kama vile uvuvi na usafiri wa majini. Bi Monica alisema, TMA imeendelea
kuhakikisha mchango wa wanahabari utambulika kwa kushirikisha wadau mbalimbali
wa kuongeza thamani za Tuzo za Wanahabari wa Masuala ya Hali ya Hewa nchini.
Ushirikiano katika tuzo hizi ni sehemu ya juhudi za
kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia
na vyombo vya habari katika kuimarisha uelewa,usambazaji na matumizi ya taarifa
za hali ya hewa katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii.






.jpeg)


.jpeg)
Post a Comment