TRA YAPONGEZA UTENDAJI WA FORODHA KASUMULU, YAKUSANYA MAPATO ZAIDI KWA MIEZI 10 MFULULIZO

******
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Uledi Abbas Mussa na menejimenti ya TRA ikiongozwa na Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda imefanya ziara mkoani Mbeya na kutembelea mpaka wa Kasumulu ambako shughuli za Forodha zinaendelea kama kawaida.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mei 22, 2026, Mwenyekiti wa Bodi Bw. Uledi amewapongeza watumishi waliopo kwenye kituo cha Forodha cha Kasumulu pamoja na watumishi wa Taasisi nyingine za Serikali waliopo mpakani hapo kwa kuwezesha ukusanyaji wa mapato ya Forodha. 

Amesema mazingira ya Tanzania ni mazuri kibiashara na utulivu katika masuala ya kodi, hali inayowavutia nchi zinazoizunguka Tanzania kutumia Bandari za Tanzania. 

"Nawapongeza kwa kujenga uhusiano mzuri na Walipakodi na kuwezesha biashara na huduma za forodha katika mpaka wa Kasumulu hali ambayo imewawezesha kuvuka malengo ya makusanyo mliyowekewa na Serikali kwa miezi 10 mfululizo ya mwaka wa fedha 2025/2026" amesema Uledi. 

Awali akizungumza Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mwenda amesema wataendelea kushirikiana na wafanyabiashara kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara, kuwezesha biashara na kurahisisha ulipaji wa kodi. 

Bw. Mwenda amewashukuru Walipakodi mkoani Mbeya kwa kuwa waaminifu katika ulipaji wa kodi na kulipa kwa wakati na kuwataka wawafichue watu wanaokwepa kodi kwani wamekuwa wakidhoofisha biashara zao. 

Naye Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha amesema TRA ipo kwaajili ya walipakodi na itaendelea kuwezesha biashara zao na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa Mamlaka hiyo na kueleza pale wanapokutana na changamoto ili zipatiwe ufumbuzi. 






Mwisho.
 

0/Post a Comment/Comments