TRA YATOA UFAFANUZI KUHUSU MALALAMIKO YA KUCHOMA MOTO GARI

******

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa kwa Mhe. Waziri Mkuu tarehe 23.05.2026 na Ndugu Odilo Boniface Ngamilaga kuhusiana na gari namba T.548 AYD aina ya Toyota Hilux Surf 4 Runner Sports kudaiwa kuchomwa moto na TRA.

Kwa mujibu wa taarifa sahihi zilizopo Gari linalolalamikiwa ni mali ya Holiday Beach Resorts Company Limited na lilikamatwa tarehe 23 Mei, 2013 na Ofisi ya TRA Mkoa wa Iringa likiwa na ndg Odilo Boniface Ngamilaga kutokana na ukiukwaji wa taratibu za forodha ikiwemo kutolipiwa kodi stahiki.

Baada ya kukamatwa kwa gari hilo, mhusika aliyekutwa nalo alitakiwa kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha umiliki na mauziano ya gari ili kuwezesha ukokotoaji na ulipaji wa kodi pamoja na kukamilisha taratibu za kiforodha lakini nyaraka hizo hazikuwahi kuwasilishwa kwa TRA.

Mnamo tarehe 06.05.2014 gari hilo liliungua moto katika eneo la Ofisi za TRA Iringa majira ya usiku katika mazingira ya kutatanisha na wakati tukio hilo linatokea, taratibu za kiforodha pamoja na uthibitisho wa umiliki wa gari hilo zilikuwa bado hazijakamilika.

Kutokana na tukio hilo, mlalamikaji alifungua shauri mahakamani dhidi ya TRA na kudai fidia lakini shauri hilo liliamuliwa kinyume yake kupitia Hukumu Na. 42/2016 iliyotolewa tarehe 25 Aprili, 2017 ambapo mlalamikaji alishindwa kesi baada ya kushindwa kuthibitisha umiliki wa gari hilo.

Aidha, kutokana na maelekezo ya Mh. Waziri Mkuu, TRA itaendelea kumsikiliza mlalamikaji ili kupata ufumbuzi kwa MUJIBU WA MATAKWA YA SHERIA. 

TRA inapenda kuwahakikishia wananchi ambao mali zao zipo katika ufuatiliaji wa uwajibikaji wa kikodi chini ya TRA kuwa haki ya Mali zao zinalindwa na zipo salama.

Mamlaka inapenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wananchi wote wenye malalamiko ya aina hii na yanayofanana na hili kuwasilisha malalamiko yao kwenye ofisi za TRA zilizo karibu nao ili yapatiwe ufumbuzi wa haraka.

Imetolewa na:

Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)


“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
 

0/Post a Comment/Comments