UFALME WA MUNGU WAFIKA DODOMA, VIJANA WATAKIWA KUMCHA MUNGU

.............

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Mwimbaji wa nyimbo za injili Dr. Ipyana Kibona ametoa wito kwa vijana nchini kumtanguliza Mungu katika maisha yao badala ya kukimbilia vitu vya dunia, akisisitiza kuwa mafanikio ya kweli yanapatikana kwa kumtafuta Mungu na kuishi katika haki yake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada ya kuwasili kwa ajili ya maandalizi ya ibada kubwa ya kusifu na kuabudu ya The Kingdom Has Come itakayofanyika Mei 22 na 23 katika Viwanja vya Wajenzi, Dodoma, Dkt. Ipyana alisema vijana wengi wanahangaika kutafuta mafanikio sehemu zisizo sahihi huku wakisahau msingi mkuu wa maisha ambao ni kumcha Mungu.

Akinukuu Biblia katika kitabu cha Zaburi 34:9-10, alisema: “Mcheni Bwana enyi watakatifu wake, maana wamchao hawatahitaji kitu.”

“Vijana wangu tunachokitafuta hakipo huko nje. Tunapaswa kutafuta kwanza ukuu wa Mungu na haki yake, mengine yote tutazidishiwa,” alisema.

Dkt. Ipyana alisema anashukuru kuona kizazi kipya cha vijana wanaompenda Mungu kikiendelea kuibuka nchini, akieleza kuwa kizazi hicho hakina mipaka ya umri wala mazingira kwa sababu Mungu mwenyewe anakipa nguvu ya kusimama madhabahuni na kumtangaza duniani.

Alisema ibada hiyo itakuwa ya kipekee kwa kuwa mbali na kusifu na kuabudu, kutakuwa na maombi makubwa, miujiza pamoja na kuguswa kwa maisha ya watu kupitia nguvu za Mungu.

“Niwahakikishie kwamba tutacheza sana, tutaruka sana lakini zaidi tutamuomba Mungu na kumsifu kwa nguvu zote. Hii ndiyo wiki yetu ya kwenda salama kwa sababu ufalme wa Mungu umefika Dodoma,” alisema.

Aidha, alisema maandalizi ya ibada hiyo yamefanyika kwa zaidi ya mwezi mmoja kwa maombi na maandalizi mbalimbali, huku akishukuru mapokezi makubwa kutoka kwa wakazi wa Dodoma.

Kwa mujibu wa Dkt. Ipyana, ujumbe mkuu wa ibada hiyo ni kumuinua Yesu Kristo ili watu wamrudie Mungu na kuishi sawasawa na mapenzi yake.

“Tunapomsifu Mungu na kumuabudu, anakuja katikati ya sifa za watakatifu wake na hapo ndipo mambo mbalimbali yanaanza kurekebishwa. Kutakuwa na miujiza, uponyaji, laana zitavunjwa na watu watafunguliwa kutoka kwenye vifungo vya muda mrefu,” alisema.

Aliongeza kuwa ibada hiyo inalenga pia kuhamasisha vijana kuishi katika hofu ya Mungu na kujiepusha na matendo yanayoharibu maisha yao na mustakabali wa taifa.

Kwa upande wake, mchungaji Dkt. Linus Marco alisema lengo la mkusanyiko huo ni kumpokea mtumishi wa Mungu Dkt. Ipyana Kibona ambaye amebeba maono ya Grand Ibada Global pamoja na Dr. Ipyana Foundation.

Aliwataka vijana wa Tanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki ibada hiyo huku wakizingatia misingi ya amani, upendo na mshikamano ambayo taifa la Tanzania linaisimamia.

“Neno la Mungu linapokaa ndani ya vijana, linawasaidia kuwa nuru ya ulimwengu na kuwa chachu ya mabadiliko mema katika jamii,” alisema.

Naye kijana Careen Lomayan aliwataka vijana kuishi maisha ya kumcha Mungu wakiwa bado katika umri wa ujana ili kuepuka majuto ya baadaye.

“Tukichezea ujana wetu leo, maisha yetu ya baadaye yatakuwa na shida nyingi. Vijana tunapaswa kuishi katika mapenzi ya Mungu na kuachana na matendo yanayoenda kinyume na mapenzi yake,” alisema.

Kwa upande wake, kijana Andrew Mwambalaswa aliwahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi katika ibada hiyo akisema madhabahu ni sehemu ya kupata ulinzi, amani na mwelekeo sahihi wa maisha.

“Njoo umpate Mungu wakati wa ujana wako. Tunaamini kupitia ibada hii vijana wengi wataepukana na changamoto zinazolikumba kizazi cha sasa cha Gen Z,” alisema.

Ibada ya The Kingdom Has Come inatarajiwa kuwakutanisha maelfu ya waumini na vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania katika Viwanja vya Wajenzi jijini Dodoma.






 

0/Post a Comment/Comments