Njombe
Wamiliki wa ardhi ambao maeneo yao yamepangwa na kupimwa wanawajibika kulipa Kodi ya Pango la Ardhi tofauti na ilivyozoeleka kuwa wanaopaswa kulipa Kodi hiyo ni wale wenye hati milki za ardhi.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 7 Mei, 2026 na Kaimu Afisa Maendeleo ya Ardhi katika Halmashauri ya Mji Njombe, Bw. Emanuel Amos kupitia kipindi kilichorushwa na redio Kings fm mkoani Njombe.
"Kwa mujibu ya Sheria ya Ardhi Namba 9 ya Mwaka 1999 na marekebisho yake kila kipande cha ardhi kikishapimwa hata kama huna nyaraka ya umiliki unapaswa kulipa Kodi ya pango la ardhi pale tu eneo lako linapokuwa limeidhinishiwa upimaji wake baada ya siku tisini ". Amesema Bw. Amos
Ameeleza kuwa, wale wote wenye ardhi lakini hawana nyaraka ila maeneo yao yamepimwa na viwanja au mashamba kuidhinishwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wanapaswa kulipa Kodi hiyo ya Ardhi.
Kwa mujibu wa Bw. Amos, mtu anapomilikishwa ardhi anakuwa ni mpangaji wa serikali, hivyo anawajibika kulipa kodi ya pango la ardhi kulingana na masharti yaliyowekwa kisheria.
Amesema, kiwango cha kodi hiyo ya pango la ardhi hutozwa kulingana na matumizi ya ardhi, ukubwa wa kiwanja pamoja na thamani ya ardhi ya eneo husika.
Bw, Emanuel alitumia pia fursa ya kipindi hicho cha redio kuwaeleza wananchi tofauti kati ya namba ya kiwanja na Namba ya nyumba.

Post a Comment