*******
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wakati matumizi ya mitandao ya kijamii yakiendelea kukua kwa kasi na kuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kijamii na kiuchumi, changamoto ya matumizi mabaya ya majukwaa hayo imeanza kuibua wasiwasi kwa jamii huku Jeshi la Polisi likionya na kuanza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi, Dodoma,pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kudhibiti uhalifu kupitia ushirikiano na wananchi, bado kuna baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya vitendo vinavyokiuka maadili na sheria, ikiwemo utapeli, matusi, udhalilishaji na uchochezi.
Jeshi hilo limeeleza kuwa hali ya usalama nchini inaendelea kuwa shwari, huku matukio machache ya kihalifu yakishughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Msemaji huyo anebainisha kuwa wahusika wa makosa ya mtandaoni wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, ambayo imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kudhibiti uhalifu wa kidijitali nchini.
Amefafanua kuwa Katika operesheni za hivi karibuni, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu katika mikoa ya Arusha, Iringa na Mbeya kwa tuhuma za kutumia vibaya mitandao ya kijamii, ikiwemo kutoa lugha za matusi dhidi ya watu mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Tume ya Uchunguzi wa matukio ya vurugu za Oktoba 29, 2025.
Aidha, Jeshi hilo limeeleza kuwa msako dhidi ya watuhumiwa wengine unaendelea, hasa wale wanaohusika katika kusambaza maudhui ya kashfa, chuki na upotoshaji wa taarifa, hata kama si waanzilishi wa maudhui hayo.
Katika hatua nyingine,jeshi hilo limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kudhibiti uhalifu huo, huku wakihimizwa kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuzingatia sheria za nchi.
Aidha jeshi la Polisi limesisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka sheria, bila kujali nafasi au hadhi yake katika jamii.

Post a Comment