Na Carlos Claudio, Dodoma.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amekemea vitendo vya “kamata kamata” ya wananchi na vitendea kazi vyao bila sababu za msingi, akisema tabia hiyo ni ya kizamani na inarudisha nyuma jitihada za wananchi kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza leo Mei 17, 2026 katika ziara yake ya kikazi wilayani Chemba mkoani Dodoma, Waziri Mkuu amesema wananchi wanapaswa kuishi kwa amani, uhuru na usalama huku akimtaka Mkuu wa Mkoa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha haki za wananchi zinalindwa.
“Kamata kamata isiyo na sababu za msingi haya ni mambo ya zamani. Mwananchi ndiye mshiriki na mlinzi wa kwanza wa vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo wananchi wanapaswa kuheshimiwa na kusikilizwa,” amesema.
Amesema si sahihi kuwashikilia wananchi vitendea kazi vyao kwa makosa madogo huku wakitegemewa kuzalisha uchumi na kuendesha maisha ya familia zao.
“Sio tu kamata kamata ya raia, hata kushikilia vitendea kazi ni mambo ya kizamani. Mtu anafanya shughuli halali ya kumletea kipato sasa mnashikiliaje kifaa chake? Atafanyaje kazi?” amehoji.
Waziri Mkuu alitoa mfano wa gari lililoshikiliwa eneo la Mvumi kwa faini ya Shilingi laki saba huku thamani ya gari hilo ikiwa ni zaidi ya Shilingi milioni 27, akisema hatua hiyo ni ya kupuuza juhudi za wananchi kujitafutia maisha.
“Ukichukua kitendea kazi cha mtu ambaye hajaajiriwa umeua familia nzima. Unataka akulipe lakini unamshikilia kifaa chake cha kazi, atalipaje?” amesema.
Aidha, amesema Serikali imepokea maelekezo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufuta sheria ya kutaifisha mali ili kulinda haki za wananchi na kuweka mazingira bora ya uzalishaji na ukuaji wa uchumi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake huku miradi ya maendeleo ikipewa kipaumbele ili kubadilisha maisha ya Watanzania.
Amesema Serikali ya Rais Samia imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, ambulansi zenye hadhi ya ICU, pamoja na shule za amali 103 ambapo shule 29 ni za mkondo wa uhandisi.
Pia amesema Serikali imenunua mitambo ya uchimbaji maji kwa kila mkoa ili kuimarisha huduma za maji huku miradi ya umeme ikiendelea kutekelezwa, ikiwemo mradi wa kuimarisha gridi ya taifa uliogharimu Shilingi trilioni 1.1 ili kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.
“Tumeweka mkakati kuhakikisha wakandarasi wanalipwa ili miradi iliyosimama iendelee na ile iliyosuasua irejee kwenye kasi yake,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema ziara za Waziri Mkuu zimeendelea kurejesha matumaini kwa wananchi huku viongozi wa mkoa wakiahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.
“Sisi Mkoa wa Dodoma tumekuja na kaulimbiu inayosema ‘Kero yako, Uwajibu wangu, Tabasamu na Samia’, na tumejipanga kuhakikisha changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi,” amesema.
Naye Mbunge wa Chemba, Kunti Majala amesema pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi, bado kumekuwa na matukio ya wananchi kukamatwa bila sababu za msingi na kupewa kesi za uzurulaji.
“Wananchi wetu ni wastaarabu, wakipewa elimu wanaelewa. Lakini mtu anakamatwa akiwa kwenye kibanda chake anapika na kupelekwa kituo cha polisi, hali hii inaleta hofu kwa wananchi,” amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Jesca Mbogo ameomba Serikali kusaidia kutatua changamoto ya utolewaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisema baadhi ya halmashauri bado hazitengi fedha hizo kwa wakati.
@Mussa







Post a Comment