Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha mikakati ya kudhibiti migogoro kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu nchini kupitia hatua mbalimbali za uhifadhi na ushirikishwaji wa wananchi. Hayo yamejadiliwa katika semina maalum iliyotolewa kwa wabunge jijini Dodoma leo Mei 12, 2026 ikiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu.
Mikakati iliyojadiliwa ni pamoja na kuimarisha Jeshi la Uhifadhi, matumizi ya teknolojia za kisasa, doria, matumizi ya ndege nyuki, visukuma mawimbi na vilipuzi vyenye pilipili kufukuza tembo, kujenga vituo vya askari, vizimba vya mamba na viboko, mabwawa ya maji pamoja na kutumia uzio wa umeme katika maeneo yenye changamoto pamoja na utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, kuboresha matumizi ya ardhi vijijini na kuimarisha mfumo wa kifuta machozi kupitia mfumo wa kidigitali wa PAIS.
Pia, Semina hiyo ilijadili mpango wa ujenzi wa Makumbusho ya Marais Wastaafu katika eneo la Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kuhifadhi historia, kumbukumbu na urithi wa viongozi wakuu waliowahi kuliongoza Taifa pamoja na kuimarisha utalii wa kihistoria na kiutamaduni nchini.
Aidha, Waheshimiwa wabunge wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa namna inavyoendelea kukabiliana na migogoro kati ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuitaka Wizara kuongeza jitihada katika kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini ikiwemo kuendeleza mikakati zaidi ya kukabiliana na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu.







Post a Comment