BALOZI MULAMULA- WANAWAKE NI NGUZO MUHIMU KUDUMISHA AMANI NA USALAMA WA AFRIKA

*****

Balozi Liberata Mulamula ametimiza mwaka mmoja tangu kuteuliwa katika nafasi ya Mjumbe Maalum wa Wanawake katika Umoja wa Afrika (AU), ambapo amesisitiza umuhimu wa wanawake katika kudumisha amani na usalama kwa jamii ya Afrika.

Balozi Liberata Mulamula ametoa msisitizo huo, alipokuwa akifanya mahojiano maalumu kuhusu utendaji wake wa mwaka mmoja tangu kuteuliwa katika nafasi hiyo ya wanawake Afrika.

"Wanawake ni nguzo muhimu katika kudumisha amani na usalama, ni lazima wahusishwea na kushirikishwa katika mipango na maamuzi mbalimbali yanayofanyika kuanzia ngazi ya jamii, taifa na kimataifa.

"Hiki ndicho ofisi yangu imekuwa ikikifanya tangu niingie, lengo la kuanzishwa ofisi hii ya wanawake AU, ni kuhakikisha inawainua wanawake kutoka katika vikwazo na vizuizi mbalimbali vilivyokuwa vinawazuia wanawake kushiriki ipasavyo maamuzi ya kutafuta amani na usalama,"alisema.

Alisema katika kipindi chake cha mwaka mmoja wa uongozi, amehakikisha anasukuma agenda hiyo ya ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi mbalimbali ikiwemo kisiasa, kiuchumi na kijamii, msisitizo ukiwa kukomesha masuala ya ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia.

Pia, amesisistiza kuwa anaendea kuweka msukumo kwa viongozi na serikali za mataifa ya Afrika ambao ni wanachama wa AU, kuhakikisha wanaweka sera nzuri za kuwainua wanawake na kuwaendeleza kushiriki vyema katika maamuzi mbalimbali.

"Hakuwezi kuzungumzia usalama na amani ya Afrika bila kuwashirikisha na kuwahusisha wanawake kikamilifu. Mara nyingi katika migogoro wanawake wanatajwa kama wahanga jambo ambalo siyo sahihi, bali wanawake ni washiriki muhimu katika maamuzi ya agenda mbalimbali, siyo wanga tu kama wanavyotajwa mara nyingi,"alisema.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja anajivunia hatua kubwa iliyopigwa na ofisi yake ya kufanya mijadala mbalimbali na kushiriki kikamilifu na viongozi wengine kutafuta usuluishi wa migogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Vilevile, alitolea mfano kwa maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania, katika kutekeleza kwa vitendo sera ya usawa wa kijinsia na kuvunja miiko ya muda mrefu ya uongozi ambapo,  walimchagua Rais wa kwanza Mwanamke Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na kuwa na Waziri wa kwanza mwanamke wa Wizara ya ulinzi katika awamu iliyopita, ikiwa ni mafanikio makubwa.

 

0/Post a Comment/Comments