Na Ester Maile Dodoma
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepoteza mwelekeo wa kisiasa na kujigeuza kuwa chama cha wanaharakati badala ya kuendesha siasa za ushindani wa kidemokrasia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo 13 June jijini Dodoma, Kihongosi amesema viongozi wa CHADEMA wamejikita zaidi katika harakati na kauli zinazochochea mjadala wa kisiasa, huku wakiacha jukumu lao la msingi la kushiriki na kushindana kupitia mifumo ya kisiasa iliyopo.
"CHADEMA kimebaki kuwa chama cha wanaharakati, kinaendeshwa kwa misingi ya uanaharakati. Kauli na matendo ya viongozi wao yanaonyesha wazi mwelekeo huo," alisema Kihongosi.
Ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa CCM, chama hicho hakioneshi dhamira ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa zinazolenga kuwania uongozi na kuwatumikia wananchi kupitia taratibu za uchaguzi.
Aidha, amewataka viongozi na wanachama wa CHADEMA kurejea katika siasa za kistaarabu na kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya demokrasia.


Post a Comment