CHATANDA AUNGANA NA UWT LIWALE KUMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UCHAPAKAZI

.....

NA: MWANDISHI WETU - LIWALE

Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Liwale mkoani Lindi, umeratibu kongamano maalum la kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na uchapakazi na uwajibikaji wake ambao ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo endelevu nchini.

Kongamano hilo limefanyika wilayani humo Juni 13, 2026, ambapo Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda alikuwa Mgeni Rasmi.

Katika kongamano hilo, Chatanda amesema Rais Dk. Samia amekuwa kiongozi wa mfano, si tu ndani ya nchi yetu lakini hata nje ya nchi. 

Aidha, amesisitiza kuwa utendajikazi na uwajibikaji wa Rais Dk. Samia pamoja na wasaidizi wake umekuwa chachu ya kukuza maendeleo nchini, hivyo basi, uongozi wa UWT wilayani humo umeona ni jambo jema kuandaa kongamano hilo ikiwa ni njia ya kumpongeza na kumtia moyo Rais ili aendelee kuchapakazi zaidi.

"Rais wetu mpendwa Dk. Samia ameimarisha diplomasia ya kiuchumi na mataifa mengi duniani, ambapo kutanufaika sana katika maeneo ya biashara na uwekezaji. Ziara yake nchini Urusi na ujio wa Rais wa Singapore hapa Tanzania, umefungua kurasa mpya na kuongeza ushirikiano kwa kusaini mikataba ya maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili," amesema Chatanda.

Sambamba hilo, Chatanda amesema Rais Dk. Samia anatekeleza ahadi zake kwa vitendo na ndiyo maana ndani ya siku 100 tangu aingine madarakani, amewezesha kupatikana kwa ajira 12,000 za kada za afya na ualimu, kuanza kwa bima ya afya kwa wote, huku vijana wakiwezeshwa mikopo ya shilingi bilioni 200.

"Sasa hivi fursa za ajira zimeongezeka, Rais anaendelea kutoa vibali vya ajira ili vijana wapate ajira. Pia, kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo na mataifa mengine, nchi yetu inapata upendeleo wa kupewa fursa za ajira ili vijana wa Kitanzania wakafanye kazi nje ya nchi kwa uratibu wa Balozi zetu zilizopo nje ya nchi," amesema.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Lindi, Bi. Kuruthumu Runje amesema UWT hawawezi kunyamaza pale Rais anapofanya mambo mazuri ya kimaendeleo, na ndiyo maana wameandaa kongamano hilo ikiwa ni njia ya kutambua kazi nzuri anazofanya zinazoleta tabasamu kwa wananchi.

Katika kongamano hilo, Bi. Runje alimkabidhi Chatanda tuzo ya pongezi kwa niaba ya Rais Dk. Samia ikiwa ni njia ya kutambua juhudi zake za kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.

Aidha, baadhi ya wanachama wa CCM na wananchi waliohudhuria kongamano hilo, wamesema Rais Dk. Samia amegusa maisha ya wananchi na kuwezesha kutolewa kwa mikopo ya asilimia 10. Vilevile, utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, kuboresha kwa huduma za jamii kama elimu, afya, maji, umeme na barabara.




 

0/Post a Comment/Comments