DC MSANDO ATOA SIKU TATU KUFUNGA STENDI BUBU, AWAELEKEZA WAFANYABIASHARA KUHAMIA STENDI YA MAGUFULI

.......

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amewataka wananchi wote wanaofanyia shughuli zao katika stendi bubu, hususan zilizopo kandokando ya Barabara ya Morogoro na maeneo mengine yanayotumika kupakilia abiria na mizigo, kuhamishia shughuli zao katika Stendi ya Magufuli ambayo imeelezwa kuwa na miundombinu na mazingira rafiki kwa shughuli za usafirishaji na biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17, 2026 Ofisini kwake, kuhusu maazimio muhimu yaliyopitishwa katika kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya, Msando amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha utaratibu wa biashara, kuongeza mapato ya Halmashauri na kuboresha usimamizi wa shughuli za usafiri na uchumi kwa ujumla.

Amesema Stendi ya Magufuli ina nafasi ya kutosha kwa wafanyabiashara na watoa huduma wote wanaotumia stendi zisizo rasmi, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kufanya shughuli hizo katika maeneo yasiyotambuliwa kisheria.

Katika hatua nyingine, Msando ametoa siku tatu kwa watu wanaoendesha shughuli za upakiaji wa abiria na mizigo katika maeneo ya Magari Saba, kwa Yusuph na maeneo mengine yanayotumika kama stendi zisizo rasmi kuondoka mara moja kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

Amesema kuanzia Jumatatu ijayo saa 12 asubuhi, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na taasisi nyingine husika zitaanza operesheni ya kuwaondoa wote wanaoendelea kutumia maeneo hayo kama stendi bubu na kuhakikisha shughuli zote zinafanyika katika vituo rasmi vilivyotengwa.

Msando ameeleza kuwa Serikali imeamua kulishughulikia kwa uzito suala la stendi bubu kutokana na athari zake kwa usalama, ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa shughuli za usafiri, akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia maeneo hayo kuingia na kutoka nchini bila kufuata taratibu za kisheria.

Aidha, amezitaka taasisi zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi na uanzishwaji wa maeneo ya biashara kuwajibika ipasavyo ili kudhibiti chanzo cha tatizo hilo badala ya kushughulikia matokeo yake pekee.

Amesisitiza kuwa tatizo la stendi bubu lina vyanzo mbalimbali vinavyohitaji kushughulikiwa kwa pamoja na wadau wote husika, huku akieleza kuwa Serikali haitalichukulia suala hilo kama changamoto isiyokuwa na ufumbuzi bali itaendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kurejesha utaratibu katika sekta ya usafiri na biashara.



0/Post a Comment/Comments