DCB YAZINDUA KAMPENI YA TUMA BURE, SHINDA KILA WIKI

******

Na Mwandishi Wetu

Benki ya DCB imezindua kampeni maalum ya miezi sita ijulikanayo kama *“Tuma Bure, Shinda Kila Wiki”* yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali na kuongeza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi wa benki hiyo walisema inalenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia mifumo ya kisasa ya kifedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Sabasaba Moshingi, alisema kampeni hiyo inaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma rasmi za kifedha kwa urahisi.

Alisema benki hiyo imeendelea kuboresha huduma zake za kidijitali ili kukidhi mahitaji ya wateja wanaotaka huduma za haraka, salama na zinazopatikana muda wote.

Kwa mujibu wa Moshingi, tafiti zilizofanywa na benki hiyo zimebaini kuwa wateja wengi wanahitaji huduma zenye gharama nafuu na zinazorahisisha upatikanaji wa huduma za benki.

Kutokana na matokeo hayo, DCB imefanya maboresho ya mifumo yake ya kidijitali ikiwemo DCB Pesa App inayowawezesha wananchi kufungua akaunti na kufanya miamala popote walipo nchini.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuwafikia wateja wengi zaidi bila kulazimika kutembelea matawi.

Mkuu wa Idara ya Masoko wa DCB, Geofrey Magugi, alisema wateja watakaofungua akaunti kupitia DCB Pesa App na kufanya angalau muamala mmoja wataingia kwenye droo za kila wiki.

Alieleza kuwa washindi 10 watajishindia Sh100,000 kila mmoja kila wiki, huku wanaofanya miamala zaidi ya mitatu kwa mwezi wakipata nafasi ya kushinda Sh milioni moja kila mwezi.

Naye Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Ramadhani Mganga, alisema kampeni hiyo itakamilika Desemba mwaka huu na itahusisha zawadi za kila wiki, kila mwezi pamoja na zawadi kubwa ya mwisho kwa washiriki watakaotumia huduma za kidijitali za benki hiyo.














 

0/Post a Comment/Comments