HOSPITALI YA BENJAMINI MKAPA YAENDELEA KUTOA HUDUMA YA UPANDIKIZAJI WA UBOHO KWA WAGONJWA WA SIKO SELI

.......

Na Ester Maile, Dodoma

Hospitali ya Benjamini Mkapa inaendelea kutoa huduma ya upandikizaji wa uboho kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa siko seli, ambapo inakadiriwa kuwa wagonjwa takribani elfu tatu huugua ugonjwa huo kila mwaka. Aidha, Tanzania inatajwa kuwa nchi ya nne duniani na ya tatu barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa siko seli.

Hayo yamebainishwa leo, Juni 25, 2026, jijini Dodoma na Dkt. Happiness Igogo, daktari bingwa wa magonjwa ya damu, wakati akizungumza na wahariri katika mkutano uliofanyika katika Hospitali ya Benjamini Mkapa.

Dkt. Igogo ameeleza kuwa ugonjwa wa siko seli ni ugonjwa wa kurithi, ambapo mtoto anaweza kuurithi kutoka kwa wazazi wake. Amesema kuwa wazazi wote wawili wanapokuwa na vinasaba vya ugonjwa huo, wanaweza kupata mtoto mwenye ugonjwa wa siko seli.

Hata hivyo, Hospitali ya Benjamini Mkapa imeendelea kuwa suluhisho kwa wagonjwa wa ugonjwa huo kupitia huduma ya upandikizaji wa uboho. Mpaka sasa, hospitali hiyo imefanikiwa kutibu wagonjwa 31 wa siko seli, huku wagonjwa 30 wakipona kabisa na kurejea kuendelea na masomo pamoja na shughuli zao za kawaida.




 

0/Post a Comment/Comments