HOSPITALI YA MALINYI YANUFAIKA NA MSAADA WA KIJAMII KUTOKA WRRB


Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na udanganyifu na uchakachuaji wa taarifa katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kusisitiza itaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha misingi ya uadilifu na uwazi inazingatiwa ipasavyo.

Bangu,ametoa onyo hilo baada ya kufanya kikao kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, kilichohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Amesema mfumo huo unaendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwazi, huku WRRB ikiendelea kushirikiana na mamlaka za mikoa, wilaya na halmashauri kusimamia utekelezaji wake.

“Moja ambalo nataka kuliweka wazi kwa Watanzania ni kwamba mfumo huu unafanya kazi kwa kuzingatia uadilifu. Kuna maeneo mengi mfumo unafanya vizuri, lakini tumeanza kuona baadhi ya watu wakiingiza taarifa zisizo sahihi kwenye mfumo kwa lengo la kujipatia fedha. Nataka nitoe onyo kali kwao kwamba tunasimamia mfumo huu kwa karibu na hatua stahiki zitachukuliwa,” amesema Bangu.

Ameeleza kuwa WRRB imeweka utaratibu wa kufanya uhakiki wa bidhaa zilizopo maghalani kabla ya kutolewa kwa katalogi za mauzo ili kuhakikisha wanunuzi wanapata taarifa sahihi kuhusu kiasi cha mazao yaliyopo.

Bangu pia amewahamasisha wakulima wa ufuta kuendelea kuuza mazao yao kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kupata masoko yenye ushindani na kuongeza kipato chao.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara ya mazao kupitia mfumo huo, jambo linalowezesha wakulima kunufaika zaidi na jasho lao.

“Wilaya ya Malinyi imeonyesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mfumo huu. Miaka michache iliyopita kulikuwa na changamoto, lakini sasa tumeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha wakulima wananufaika na mapato yao yanaongezeka,” amesema.

Katika hatua nyingine, WRRB imekabidhi msaada wa vifaa vya usafi na vyakula kwa Hospitali ya Wilaya ya Malinyi ikiwa ni sehemu ya shughuli zake za uwajibikaji kwa jamii.

Akikabidhi msaada huo katika Wodi ya Wazazi ya hospitali hiyo, Bangu amesema WRRB itaendelea kushirikiana na jamii sambamba na kutekeleza majukumu yake ya kusimamia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Dk. Julius Nyasongo, aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Wakili Sebastian Waryuba, ameishukuru WRRB kwa msaada huo akisema utasaidia kuboresha ustawi wa akina mama wanaopata huduma hospitalini hapo.

“Msaada huu utakuwa na mchango mkubwa kwa akina mama wanaopata huduma katika hospitali yetu. Tunawashukuru WRRB kwa kuendelea kushirikiana na sekta ya afya na jamii kwa ujumla,” amesema Dk. Nyasongo.

0/Post a Comment/Comments