ISW Kufanya Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Ustawi wa Jamii


 *******

Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) kimetangaza kufanyika kwa Kongamano lake la kwanza la kimataifa la Uwezeshaji wa Watu na Ustawi wa Jamii litakalofanyika Juni 5, 2026 katika Ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni, alisema kongamano hilo lenye kaulimbiu ya “Kuwawezesha Watu na Kubadilisha Jamii: Njia za Kufikia Ustawi Endelevu”litawakutanisha wataalamu, watafiti, watunga sera na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Dkt. Nyoni alisema washiriki kutoka nchi 11 zikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya, Nigeria, Namibia, Lesotho, Austria, Zimbabwe, Afrika Kusini, Norway na Hungary wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo wa siku moja.

Alisema kongamano hilo litahudhuriwa pia na wataalamu mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali watakaowasilisha mada zinazohusu uwezeshaji wa wanawake, haki za watoto, afya ya akili, elimu ya fedha, ujasiriamali na maendeleo ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Dkt. Nyoni, mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa, uzoefu na matokeo ya tafiti yatakayosaidia kuimarisha ustawi wa jamii na maendeleo jumuishi ndani na nje ya Tanzania.

Alisema kongamano hilo limeandaliwa katika kipindi muhimu kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi wa kati wa juu unaowanufaisha wananchi wote.

“Tunataka kongamano hili liwe sehemu ya majadiliano ya awali yatakayochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kupitia ushahidi wa kisayansi, tafiti na ushauri wa kitaalamu,” alisema Dkt. Nyoni.

Aliongeza kuwa mapendekezo yatakayotokana na kongamano hilo yatawasilishwa kwa wizara na taasisi husika ili kusaidia utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo, huku akiwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kufuatilia mijadala hiyo kupitia majukwaa ya mtandao.



0/Post a Comment/Comments