Na Mwandishi wetu,Dodoma.
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ni moja ya nyenzo muhimu zinazotumiwa na mataifa mengi duniani kuongeza ufanisi wa taasisi za umma, jambo ambalo limekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi.
Kafulila ameyasema hayo leo Juni 3,2026 wakati wa Muhadhara wa Umma ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambapo amesema duniani zipo sababu kuu tatu zinazochochea matumizi ya mfumo wa PPP.
Ametaja sababu hizo kuwa ni kuvutia mitaji ya sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya umma, kuongeza ufanisi wa taasisi na kukuza ubunifu.
Amesema uzoefu wa kimataifa unaonesha kuwa mafanikio ya kiuchumi ya mataifa mengi hayategemei rasilimali za asili pekee bali zaidi ufanisi wa taasisi zake na uwezo wa kutumia rasilimali hizo kwa tija.
“Katika baadhi ya nchi zilizoendelea, takribani asilimia 25 ya utajiri wa taifa unatokana na ufanisi wa taasisi huku rasilimali za asili zikichangia takribani asilimia tano pekee,” alisema Kafulila.
Aidha amefafanua kuwa mafanikio hayo hayamaanishi kuwa mataifa hayo hayana rasilimali za asili, bali yamewekeza katika kujenga mifumo imara inayowezesha rasilimali hizo kuchangia maendeleo kwa kiwango kikubwa zaidi.
Kafulila amesema China inaongoza kwa uzalishaji wa dhahabu kuliko nchi yoyote barani Afrika, Marekani ina akiba kubwa ya mafuta kuliko mataifa mengi duniani huku Urusi ikiwa na gesi nyingi kuliko nchi yoyote Afrika, lakini nguvu kubwa ya uchumi wao inatokana na rasilimali watu, ubunifu na taasisi zenye ufanisi mkubwa.
Amesema mfumo wa PPP unasaidia si tu kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo, bali pia kuimarisha ufanisi wa taasisi za umma na kuhamasisha ubunifu ambao ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa.
Katika hatua nyingine, Kafulila amesema matumizi ya misamaha ya kodi kwa baadhi ya sekta za uzalishaji, bado ni muhimu pale inapotoa matokeo halisi katika kuvutia uwekezaji na kupunguza gharama za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Kafulila baadhi ya uwekezaji huhitaji mtaji mkubwa wa kuanzishwa na kwamba misamaha ya kodi inaweza kusaidia kupunguza gharama hizo na kufanya mazingira ya biashara kuwa rafiki zaidi kwa wawekezaji.
Wakati huo huo, Kafulila amesema anatamani kuona Chuo Kikuu cha Dodoma kikianzisha Shahada ya Uzamili ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Masters in PPP) ili kuongeza idadi ya wataalamu wa ndani wenye ujuzi wa kusimamia miradi ya ubia.
***








Post a Comment