KILIO CHA MAJI CHAWAKUMBA WAKAZI WA CHIMALAA DODOMA, WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA KATI

......

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakazi wa Mtaa wa Chimalaa, Kata ya Ntyuka jijini Dodoma, wameiomba Serikali kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama, wakidai wanalazimika kutumia chanzo kimoja cha maji pamoja na mifugo, hali inayowatia hofu ya kuendelea kuathirika kiafya.

Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya wananchi walisema wamekuwa wakiahidiwa huduma ya maji kila kipindi cha uchaguzi, lakini hadi sasa bado wanakabiliwa na mateso makubwa ya kutafuta maji.

Mkazi wa eneo hilo, Eunice Chiwanga, alisema wananchi wa Chimalaa wanaendelea kupitia mateso makubwa kutokana na ukosefu wa huduma hiyo muhimu.

"Tunaiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wetu na viongozi wengine watuangalie.Tunatumia maji pamoja na mifugo, usiku hata fisi wanakuja kunywa. Watu wanafua, wanaoga na wengine wanachota maji hayo kwa matumizi ya nyumbani," alisema.

Naye Isabela Nhambi alisema tatizo la maji limekuwa kero ya muda mrefu huku akieleza kuwa kila kipindi cha kampeni wananchi hupewa ahadi za kupatiwa maji ambazo hazijatekelezwa.

"Kila mwaka tunaletewa ahadi za maji wakati wa kampeni, lakini mpaka leo hakuna mabadiliko. Tumechoka na ahadi. Tunachohitaji ni maji safi na salama. Hatuwezi kuendelea kutumia maji yanayotumiwa pia na mifugo," alisema.

Kwa upande wake, Ritha Mbilinyi alisema wananchi wengi wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa yanayodaiwa kusababishwa na matumizi ya maji yasiyo salama.

Alisema endapo chanzo hicho cha maji kitapungua au kukauka, wananchi hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata maji katika maeneo mengine, jambo linaloongeza ugumu wa maisha yao ya kila siku.

Akizungumzia changamoto hiyo, Diwani wa Kata ya Makulu, Theobalt Maina, alisema maeneo ya Bwawani, Chimalaa na Chidachi ndani ya Kata ya Ntyuka ndiyo yaliyoathirika zaidi na tatizo la maji.

Alitoa wito kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kutembelea kata hiyo ili kujionea hali halisi na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maji.

Maina alipendekeza Serikali ichimbe visima, ijenge matenki ya kuhifadhi maji na kusambaza mtandao wa maji katika mitaa hiyo ili kuondoa adha inayowakabili wananchi.

Aidha, alisema kuwa hivi karibuni Waziri Aweso alitoa Sh milioni 500 kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji katika eneo la Iringa, hivyo akaomba msaada kama huo utolewe pia kwa wakazi wa Ntyuka.

"Haileti picha nzuri kuona Kata ya Ntyuka, ambayo ipo takribani kilomita tano tu kutoka katikati ya Jiji la Dodoma na makao makuu ya nchi, wananchi wake bado wanakosa huduma muhimu ya maji safi na salama. Tunaomba Serikali iingilie kati haraka ili kuondoa mateso haya," alisema.

Wananchi hao wameeleza matumaini yao kuwa Serikali itachukua hatua za haraka kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama, wakisisitiza kuwa upatikanaji wa maji ni haki ya msingi kwa kila mwananchi.









 

0/Post a Comment/Comments