Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imezitaka daladala zote zinazofanya shughuli katika Kituo cha Mabasi cha Mbagala kuondoka ndani ya siku saba na kuhamia rasmi Kituo cha Mabasi ya Mwendokasi kilichopo Mbagala Rangi Tatu.
Hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa huduma katika mfumo wa mabasi yaendayo haraka (BRT), ambao Serikali inaendelea kuuimarisha.
LATRA pia imeweka zuio kwa daladala zinazofanya safari kati ya Gerezani, Kivukoni na Mbagala kushusha au kupakia abiria katika vituo vya njiani vilivyopo kwenye njia ya mwendokasi.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dkt. Habibu Suluo, amesema uamuzi huo umetokana na tathmini ya utendaji wa mradi wa BRT Awamu ya Pili baada ya ukaguzi uliofanyika Dar es Salaam.
Amesema kwa sasa huduma katika njia hiyo inatolewa na mabasi 50 pekee yanayofanya safari kati ya Kivukoni, Gerezani na Mbagala.
Dkt. Suluo amesema uwepo wa daladala katika njia hiyo umekuwa ukisababisha changamoto za kiutendaji na kudhoofisha huduma za usafiri wa mwendokasi.
Aidha, amesisitiza kuwa kuanzia sasa daladala zote lazima zitumie vituo rasmi vya mwendokasi na hazitaruhusiwa kusimama katikati ya njia kupakia au kushusha abiria.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Saidi Tunda, amesema ukarabati wa vituo vilivyoharibika unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Julai mwaka huu.
Amesema kukamilika kwa matengenezo hayo kutaboresha huduma na kuongeza ufanisi wa mfumo wa usafiri wa mwendokasi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa MOFAT, Mohamed Kassim, amesema bado kuna changamoto za hujuma dhidi ya mfumo huo, ikiwemo vitendo vya baadhi ya waendeshaji wa daladala na baadhi ya wananchi.
Ameeleza kuwa baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ununuzi wa kadi za usafiri bila kuzitumia, hali inayodaiwa kuathiri mapato na uendeshaji wa huduma.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha huduma za usafiri wa umma zinaboreshwa kwa manufaa ya wakazi wa Dar es salaam.













Post a Comment