Na Sixmund Begashe, Dodoma
SERIKALI imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori, kupitia sera, mikakati na matumizi ya teknolojia za kisasa hususani Mfumo wa Kidijitali wa Problem Animals Information System (PAIS) ambao ni sehemu ya mageuzi hayo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora alipokuwa akifungua mafunzo ya Mfumo wa PAIS kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri zaidi ya 400, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, Jijini Dodoma.
Dkt. Lobora amesema kuwa mafunzo hayo ni moja ya jitihada za Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii za kuendelea kuimarisha uhifadhi wa maliasili, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma na maendeleo ya Sekta ya Utalii, ambayo imeendelea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Taifa
Amefafanua kuwa mfumo huo utaiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi kwa wakati, kufanya uchambuzi wa matukio kwa ufanisi na kuchukua hatua stahiki kwa haraka zaidi.
"Matumizi ya mfumo huu yataongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika mchakato wa kushughulikia madai ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu," alisisitiza Dkt. Lobora.
Akielezea malengo ya mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Uendelezaji Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe amefafanua kuwa si kutumia teknolojia kwa ajili ya kurahisisha kazi za watumishi pekee, bali kuhakikisha mwananchi anapata huduma kwa wakati, kwa haki na kwa uwazi.
Naye Afisa Misitu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Rogasian Philip, pamoja na kuipongeza Wizara kwa jitihada hizo, amewataka Maafisa Ugani hao, kuzingatia matumizi sahihi ya vitendea kazi walivyopewa na kujiepusha na vitendo vya uzembe, udanganyifu, rushwa au matumizi mabaya ya mfumo.









Post a Comment