Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Dk. John Jingu, ameahidi kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na taasisi hiyo kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa watumishi ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za mahakama kwa wakati.
Dk. Jingu alitoa kauli hiyo Juni 22, 2026 jijini Dodoma wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama.
Akizungumza baada ya kupokea ofisi, alisema amepokea jukumu hilo kwa unyenyekevu, utayari na uwajibikaji, huku akisisitiza kuwa uadilifu, uweledi na uwajibikaji vitakuwa msingi wa utendaji wake.
“Nimepokea jukumu hili kwa unyenyekevu na utayari mkubwa wa kulitumikia taifa. Tutahakikisha Watanzania wanaendelea kunufaika na huduma bora za mhimili wa mahakama kwa kuzingatia uadilifu, uweledi na uwajibikaji,” alisema.
Alibainisha kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi na mipango yote iliyoanzishwa, sambamba na kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazokabili taasisi hiyo.
Dk. Jingu alisema moja ya maeneo ya kipaumbele ni kuimarisha miundombinu ya mahakama, kuboresha maslahi ya watumishi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
“Tunapozungumzia ufanisi wa huduma lazima tuzingatie matumizi ya teknolojia. Hili ni eneo muhimu katika kuhakikisha huduma za mahakama zinawafikia wananchi kwa haraka na kwa ubora unaotakiwa,” alisema.
Aidha, aliwataka watumishi wa mahakama kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano, akisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi yoyote hutegemea kazi ya pamoja.
“Bila kufanya kazi kama timu hakuna mafanikio. Ili tushinde lazima tufanye kazi kwa ushirikiano, kila mmoja akiwa na mchango wake katika kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu mstaafu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani aliyompa katika kipindi chake cha utumishi wa miaka 35 serikalini.
Prof. Gabriel alisema alipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na watumishi mbalimbali waliomsaidia kufanikisha majukumu yake tangu alipojiunga na Mahakama mwaka 2021.
Alimpongeza Dk. Jingu kwa kuaminiwa kuongoza taasisi hiyo, akieleza kuwa ni kiongozi mwenye uwezo na sifa zinazomwezesha kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utoaji haki nchini.
“Dk. Jingu ni mtu mzuri na mwenye uwezo mkubwa. Nina imani ataiongoza Mahakama mbele zaidi kwa kushirikiana na timu iliyopo,” alisema.
Prof. Gabriel alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake kuwa ni kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za mahakama, kuimarika kwa usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na kuongezeka kwa bajeti ya taasisi hiyo.
Alisema bajeti ya Mahakama imeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni, hatua ambayo imechangia kuimarika kwa utoaji wa huduma za haki nchini.
Aidha, alimshauri mtendaji mpya kuendelea kusimamia kwa karibu miradi ya maendeleo ya mahakama, kuimarisha nidhamu kwa watumishi na kudumisha ushirikiano kati ya mihimili ya dola ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi kwa wakati na kwa usawa.
Akihitimisha hotuba yake, Prof. Gabriel aliwataka watumishi wa Mahakama kuendelea kumpa ushirikiano Dk. Jingu kama walivyofanya kwake, akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa mafanikio ya taasisi hiyo katika kutekeleza jukumu lake la kusimamia haki na kuimarisha amani nchini.




Post a Comment