Na Ester Maile Dodoma
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuwa licha ya kutokuwepo kwa ugunduzi wa mafuta nchini hadi sasa, Tanzania imefanikiwa kugundua kiasi kikubwa cha gesi asilia katika maeneo ya Mtwara, Lindi na ukanda wa pwani, hatua iliyowezesha serikali kuendeleza matumizi ya nishati hiyo katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Afisa Mwandamizi wa TPDC, Ugine Isaya, amesema gesi asilia imeendelea kuwa nguzo muhimu ya nishati safi inayochangia uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
TPDC kwa kushirikiana na serikali, imefanikiwa kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya majumbani ambapo zaidi ya nyumba 2,515 katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na maeneo mengine tayari zinatumia nishati hiyo.
Aidha, amesema matumizi ya gesi asilia kwenye sekta ya usafiri yameongezeka kwa kasi, huku zaidi ya magari 15,500 yakiwa yameunganishwa na mfumo wa kutumia gesi. Pia kuna viwanda 59, taasisi 29 na vituo 17 vya kujazia gesi vinavyotoa huduma hiyo nchini.


Post a Comment