Wanawake wametajwa kuwa nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye maadili kupitia elimu ya dini, jambo linalodhihirishwa na ongezeko la ushiriki wao katika Mashindano ya Kitaifa ya Kuhifadhi na Kutafsiri Qur’ani Tukufu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, alisema mashindano hayo yamekuwa mfano mzuri wa kuwawezesha wanawake kujifunza na kuelewa mafundisho ya Qur’ani kwa kina.
Alisema mafanikio ya mashindano hayo hayatokani na kuhifadhi Qur’ani pekee, bali pia kutokana na msisitizo uliowekwa katika kujifunza tafsiri zake ili kuyaishi mafunzo yake katika maisha ya kila siku.
Dkt. Saada alieleza kuwa hatua ya kujumuisha tafsiri ya Qur’ani katika mashindano hayo itasaidia kuimarisha maadili na kukuza ustawi wa familia pamoja na jamii kwa ujumla.
Pia aliwahamasisha wanawake wenye nafasi mbalimbali za uongozi kuendelea kuunga mkono programu zinazolenga elimu ya dini kwa kuwa wao wana nafasi kubwa katika malezi ya kizazi kijacho.
Mratibu Mkuu wa mashindano hayo, Sheikh Muhammad Omary Samata, alisema mashindano hayo yamepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake na sasa yanawapa nafasi hata wanawake wanaohifadhi Qur’ani yote kushiriki.
Aliongeza kuwa mwitikio wa washiriki umeongezeka kila mwaka, hali inayoonyesha kuimarika kwa hamasa ya kujifunza Qur’ani miongoni mwa wanawake nchini.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu BAKWATA Taifa, Hajjat Shamim Khan, alisema ni muhimu kwa vijana kujifunza tafsiri ya Qur’ani sambamba na kuhifadhi ili waweze kuelewa vyema maadili ya dini yao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi, alipongeza ushiriki wa wanawake wa rika mbalimbali, akisema hatua hiyo inaonyesha kuwa elimu ya dini haina umri na inaweza kuwafikia watu wote.
Katika hatua nyingine, Hajjat Shamim aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha Muungano wa Tanzania, akisisitiza kuwa umoja, ushirikiano na mshikamano vilivyoasisiwa na viongozi wa mwanzo vinapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya taifa.



























Post a Comment