MASHIRIKA YA UMMA KUKUTANA IKULU KUTOA GAWIO

******

RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza hafla ya Siku ya Gawio 2026 itakayofanyika Juni 30, mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo itawakutanisha viongozi wa taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa kwa lengo la kuwasilisha gawio na michango mingine serikalini.

Ofisi ya Msajili wa Hazina imeeleza kuwa tukio hilo linaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha mchango wa uwekezaji wa umma katika kukuza uchumi wa taifa.

Gawio linalowasilishwa kila mwaka limekuwa likiongeza uwezo wa Serikali kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo bila kutegemea vyanzo vingine vya mapato pekee.

Fedha hizo huelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati pamoja na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

Miongoni mwa sekta zinazonufaika ni elimu, afya, maji, nishati na miundombinu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni *“Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu Kuelekea Dira 2050.”

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara, Bi. Lightness Mauki, alisema usimamizi bora wa uwekezaji wa umma una mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi.

Alisema mashirika na kampuni za umma zinapaswa kuendelea kuongeza ufanisi ili kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta tija na thamani kwa wananchi.

Kwa mujibu wake, mafanikio ya uwekezaji wa umma ni sehemu muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi shindani na maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2050.








 

0/Post a Comment/Comments