NA: MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Walipakodi na wananchi kwa ujumla wamekumbushwa umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari ili kodi hizo ziweze kuharakisha kasi ya maendeleo nchini.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar, Juni 27, 2026, katika viwanja vya Gymkhana Jijini Dar es Salaam, katika mbio za hisani za mlipakodi zilizoratibiwa na Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA) nchi nzima ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Katika hotuba yake fupi, Balozi Omar amesema, ni muhimu kwa walipakodi kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wako wa kulipa kodi kwa hairi na kwa wakati ili ziweze kufanikisha mipango ya maendeleo.
"Kila mwaka wa fedha tunaanza upya, tunapoingia Julai tunaanza safari mpya yenye malengo mazuri zaidi. Tunawatakia wafanyabiashara na wawekezaji mafanikio katika shughuli zao za kiuchumi, lakini mafanikio hayo yaende sambamba na kutimiza wajibu wa kulipa kodi kwa hiari, kwa wakati na kwa ukamilifu," amesema Balozi Omar.
Naye, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amepongeza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo baina ya mamlaka na walipakodi nchini, jambo linalochangia ongezeko la makusanyo ya kodi na hivyo kufikiwa kwa malengo ya kukuza uchumi na maendeleo.
Kimsingi, katika miaka 30 ya uwepo wa TRA nchini, umewezesha kuongezeka kwa mapato ambapo ongezeko hilo ni kutoka shilingi bilioni 531 mwaka 1996/1997 hadi kufikia shilingi trilioni 32 mwaka 2025/2026.


Post a Comment