Na Saidi Lufune, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amewataka watoa huduma za utalii nchini kuzingatia weledi, ufanisi na maarifa waliyonayo wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kazi zao ili kuitangaza vyema Tanzania na vivutio vyake hususan wakati wa huu wa maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Mhe. Chande amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo ya watoa huduma za utalii kwenye Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) yenye lengo kuimarisha ujuzi na weledi wa watoa huduma kwa wageni katika mnyororo wa thamani katika Sekta ya Utalii nchini.
Amesema utalii umeendelea kuimarika ambapo kulingana na takwimu za Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), idadi ya watalii imekua kwa asilimia 8.6 hadi kufikia watalii bilioni 1.52 mwaka 2025 ikilinganishwa na watalii bilioni 1.4 mwaka 2024.
Amesema kutokana na hatua hiyo ni vyema waendesha huduma za utalii nchini kuendelea kuwa wakarimu kwa wageni wanaotembelea katika vivutio vyetu ili kuepuka kuharibu jina la Tanzania
“Tuendeeee kuwa wakarimu tusizidiwe na yeyote, nawaomba muendee kufanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa sana.
"Jambo la AFCON ni nchi tatu, hapo kuna ushindani, kupitia ninyi tunatamani wale mashabiki wote wa mpira waje Tanzania kwanza si tu kuangalia mashindano ya mpira bali kuangalia vivutio vyetu vya utalii vilivyopo nchini na kudumisha urafiki kati yetu na wao,” alislsitiza Mhe. Chande.
Amebainisha kuwa ukuaji wa Sekta ya Utalii na Pato la Taifa unatokana na jitahada mbalimbali zinzofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuweka mazingira wezeshi katika kutangaza utalii kupitia filamu za 'The Royal Tour' na 'Amazing Tanzania' hivyo ni vyema waongoza utalii nchini kuiga mfano huo.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Ayoub Mohd Mahmoud (Mb) amesema Sekta ya Utalii kwa upande wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ina mchango mkubwa katika uchumi kwa takwimu za hivi karibuni hivyo Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutekeleza jukumu la uendelezaji wa utalii kwa kuhimiza amani, umoja na mshikamano kama nyenzo muhimu ya kuvutia watalii.
“Sisi kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tunalo jukumu katika Sekta hii ya Utalii na ndio maana mafunzo haya yamehudhuriwa pia na Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Zima Moto na Uokoaji tukiwa na jukumu la kuhakikisha pale majanga yanapotokea tuhakikishe usalama wa watu unazingatiwa, ” alisema Mhe. Mahmoud.
Awali Mkurugenzi wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Edward Kohi amesema mafunzo hayo yanatarajia kuwafikia watoa huduma za utalii zaidi ya 300 kutoka Sekta ya Umma na Binafsi katika viwanja vya ndege wakiwemo maafisa uhamiaji, wakusanya kodi, usalama, afya, watoa huduma za viwanja vya ndege, watoa huduma za kifedha, migahawa, usafirishaji na wauzaji wa maduka ya bidhaa za utalii.






Post a Comment