MICHEZO NI DAWA YA MAGONJWA, SHYCOM ALUMNI HALF MARATHON YAZINDULIWA RASMI SHINYANGA

........

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Serikali imewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kushiriki michezo na mazoezi ya viungo, ikieleza kuwa ni njia muhimu ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha afya ya akili, kupunguza msongo wa mawazo pamoja na kuongeza tija katika shughuli za kila siku.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Njombe, Balozi Dkt. Pindi Chana, aliyemwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, katika uzinduzi wa msimu wa pili wa SHYCOM Alumni Half Marathon 2026, utakaofanyika Septemba 26, 2026 mkoani Shinyanga.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Chana alisema michezo siyo tu njia ya kujenga afya, bali pia ni fursa ya ajira na chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa michezo inapunguza magonjwa yasiyoambukiza, inapunguza msongo wa mawazo na sonona (depression), huku ikitoa ajira kwa vijana na makundi mbalimbali," alisema.

Aliwataka wananchi kuanza kujisajili mapema kwa mbio hizo zitakazofanyika chini ya kaulimbiu isemayo, "Gari Limewaka, Kata Wese, Boresha Chuo Chetu SHYCOM."

Aidha, alisema Serikali imeendelea kuweka sekta ya michezo kuwa miongoni mwa vipaumbele kupitia bajeti zake, huku ikisisitiza kuwa mipango ya maendeleo ya miji na halmashauri inapaswa kuzingatia uwepo wa maeneo maalumu ya mazoezi na michezo.

"Tukiwekeza katika michezo na afya ya mwili, tutapunguza gharama za matibabu na matumizi ya dawa. Michezo inaongeza muda wa kuishi na kuboresha afya kwa ujumla," alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha SHYCOM, Dkt. John Nandi, alisema mbio hizo zina lengo la kuhamasisha afya bora, kuimarisha mshikamano wa wahitimu wa chuo pamoja na kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya taasisi hiyo.

Alisema kwa sasa chuo kimejikita katika ukarabati wa zahanati, madarasa na miundombinu mingine muhimu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

"Mchango wa wahitimu na wadau wetu ni uwekezaji mkubwa katika elimu na ustawi wa chuo. Tukilea vizuri kizazi cha sasa, tutakuwa tumeandaa nguvu kazi imara kwa ajili ya maendeleo ya taifa," alisema Dkt. Nandi.

Naye mmoja wa wahitimu wa SHYCOM, Yunus Mwahu, alisema wazo la kuanzisha SHYCOM Alumni Half Marathon ni la kipekee licha ya uwepo wa mbio nyingi nchini, kwa kuwa linaunganisha lengo la kuboresha afya na kuchangia maendeleo ya chuo.

Aliwahamasisha wananchi kushiriki mbio hizo, akibainisha kuwa mazoezi ni msingi wa afya njema, hususan katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kuhimiza umuhimu wa afya ya akili kupitia shughuli za mazoezi katika taasisi mbalimbali.

Mwahu aliwapongeza waandaaji pamoja na wadhamini waliojitokeza kuunga mkono tukio hilo, akisema mchango wao unaonesha ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi, wahitimu na Serikali katika kuendeleza elimu na afya ya jamii.

Alisema ushindi mkubwa wa SHYCOM Alumni Half Marathon siyo tu kumaliza mbio, bali ni kutimiza lengo la kuboresha chuo, kuhamasisha mazoezi na kujenga jamii yenye afya bora.



 

0/Post a Comment/Comments