Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imezindua mkakati wa miaka mitano (2026–2031) wa kuendeleza tasnia ya zao la pareto, ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa zao hilo na kuongeza kipato cha wakulima pamoja na mapato ya taifa kupitia mauzo ya nje.
Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo, Daniel Chingolo, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 16 wa Wadau wa Zao la Pareto.
Silinde amesema mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji wa maua ya pareto kutoka takribani tani 3,800 hadi tani 9,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2031.
Aidha, alisema serikali inalenga kuongeza tija ya uzalishaji kutoka wastani wa kilo 250–300 kwa hekta hadi kilo 800–1,200 kwa hekta, pamoja na kuongeza kiwango cha pyrethrin katika maua ya pareto kutoka wastani wa asilimia 1.3 hadi asilimia 2 ili kukidhi viwango vinavyohitajika katika soko la kimataifa.
Alieleza kuwa mkakati huo pia unakusudia kusajili hekta 29,240 za mashamba ya pareto katika mfumo wa COPRA MIS ili kuboresha usimamizi wa taarifa za uzalishaji, kuongeza uwezo wa usindikaji wa zao hilo kutoka asilimia 54 hadi asilimia 90, na kuongeza thamani ya mauzo ya nje kutoka dola za Marekani milioni 9 hadi dola milioni 15 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Silinde, serikali pia inalenga kuhakikisha wakulima wanapata kati ya asilimia 70 na 80 ya bei ya soko, hatua itakayoongeza motisha wa uzalishaji na kuinua kipato chao.
Ili kufanikisha malengo hayo, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kutekeleza hatua kadhaa za kimkakati, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na TARI, PCT na PAITEC ili kuzalisha kilo 15,000 za mbegu bora za pareto.
Hatua nyingine ni kukamilisha uthibitishaji wa aina mpya za mbegu zenye tija kubwa na kiwango cha juu cha pyrethrin, kutoa mafunzo kwa maafisa ugani 200 na wakulima 2,000 kuhusu kanuni bora za kilimo cha pareto pamoja na elimu ya fedha.
Pia serikali itasajili wakulima na mashamba yao ili kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za uzalishaji na biashara, kuimarisha mfumo wa upimaji wa ubora wa maua ya pareto na kuweka mfumo wa kidijitali wa utoaji wa taarifa kwa wakulima.
Vilevile, mkakati huo unahusisha ujenzi wa makaushio 129, uboreshaji wa vituo vya kukusanyia na kununulia pareto pamoja na kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Pareto utakaosaidia kuimarisha tasnia hiyo kwa muda mrefu.
Silinde alisema utekelezaji wa mkakati huo katika mwaka wa kwanza unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2.2, fedha zitakazotolewa kwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Alisisitiza kuwa mkakati huo unaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya kujenga tasnia ya pareto yenye tija, ushindani katika soko la kimataifa na manufaa makubwa kwa wadau wote, hususan wakulima.
"Kwa ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja tunaamini zao la pareto litakuwa miongoni mwa mazao muhimu ya biashara yatakayochangia kuongeza ajira, kipato cha wananchi na maendeleo ya uchumi wa taifa," alisema.
Aidha, aliwashukuru wadau wa tasnia ya pareto kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kukuza zao hilo, akieleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa pareto katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Serikali imewataka wadau wote kutumia kikao hicho kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuifanya tasnia ya pareto kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa
.



Post a Comment